3210; Mkokoteni mbele ya punda.
Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha kuna mtu umempa kazi ya kubeba mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Amatakiwa kutumia mkokoteni na punda.
Unamwelekeza mtu huyo, pakia mzigo kwenye huo mkokoteni, kisha ufunge kwenye punda na uupeleke.
Unaondoka ukiwa umemwachia maagizo hayo.
Anakupigia simu kwamba amefuata maelekezo lakini mzigo haujaweza kwenda.
Unamuuliza kwa makini, mkokoteni umeufunga kwenye punda? Anakujibu ndiyo.
Unashangazwa, maana siyo kitu cha kawaida.
Inakubidi uende ukajionee mwenyewe.
Unapofika, unakuta ameweka mkokoteni mbele ya punda, badala ya nyuma.
Hapo unajua hata angehangaika kiasi gani, punda asingeweza kuvuta mkokoteni ambao upo mbele yake.
Rafiki, hivyo ndivyo wengi wanavyokwamba inapokuja kwenye kupata fedha na utajiri.
Kuna fedha au utajiri wenyewe ambao ndiyo mkokoteni halafu kuna kile ambacho mtu anapaswa kufanya ndiyo apate fedha au utajiri, ambacho ndiyo punda.
Ukiangalia watu wote wanaohangaika na kufanya mambo mengi lakini bado hawapati fedha na utajiri, ni kwa sababu wametanguliza mkokoteni (kupata fedha) kabla ya punda (wanachopaswa kufanya).
Tuanze na mifano ili tuelewane vizuri.
Ukiangalia orodha ya mabilionea wote duniani, utaona kila sekta ina bilionea.
Teknolojia ina mabilionea.
Viwanda vina mabilionea.
Kilimo kina mabilionea.
Vyakula vina mabilionea.
Uwekezaji una mabilionea.
Nishati ina mabilionea.
Biashara za kununua na kuuza zina mabilionea.
Uzalishaji una mabilionea.
Huduma mbalimbali zina mabilionea.
Lakini unapoingia ndani zaidi, kwa kila bilionea, imemchukua miaka mingi kwenye hicho anachofanya mpaka kuweza kufikia ngazi hiyo.
Wengi sana ni zaidi ya miaka 10.
Na hata wachache ambao wamefikia ubilionea chini ya miaka 10 ya kuwa kwenye hicho wanachofanya, ubilionea wao unakuwa hautokani na faida waliyopata, bali thamani ya kampuni zao inayokua imekua sana kwa sababu ya wawekezaji wanaokuwa wameamini ni sehemu sahihi kwao kupata fedha zaidi.
Halafu sasa, kuna wenzetu na sisi ambao tunawajua kwa zaidi ya miaka 10 wanapambana na shughuli mbalimbali.
Lakini siyo tu kwamba hawajafikia ubilionea, bali hata ule utajiri wa kawaida hawajaupata.
Waangalie kwa kipindi hata cha miaka 10 tu na mtiririko wao hautatofautiana sana na huu;
Mwaka wa kwanza waliona ufugaji wa kuku utawalipa vizuri, wakafuga, ila wakakutana na changamoto.
Mwaka unaofuata wakasikia ufugaji wa bata mzinga ndiyo wenye hela zaidi, wakaingia.
Mwaka mwingine ufugaji wa kware, mwingine ufugaji wa sungura.
Mwaka mwingine wakasikia kilimo cha matikiti maji ndiyo kina utajiri wa haraka.
Mwaka mwingine wakasikia pesa ipo kwenye mpunga, mwaka mwingine nyanya, mwingine kitunguu.
Hapo bado biashara mbalimbali ambazo mtu anaingia, uza hivi, uza kile.
Bado anacheza michezo ya bahati nasibu.
Kote huko anaingia na haendi zaidi ya mwaka, kwa sababu kila anapokutana na changamoto, anaona fursa nyingine rahisi zaidi na kuiendea hiyo.
Kinachofanya watu wengi kuwa na mahangaiko mengi lakini bado wasipate fedha na utajiri ni hilo la kuweka mkokoteni mbele ya punda.
Wanajiuliza hivi; nawezaje kupata fedha nyingi kwa haraka na bila ya kufanya kazi?
Unaweza kudhani natania, lakini naweza kukuonyesha mpaka ushahidi wa jinsi watu wenye akili zao timamu wanaomba ushauri wa aina hiyo.
Mtu anakuwa na ujasiri kabisa wa kukuandikia; Hebu nishauri ni biashara gani ambayo nikiweka hela yangu naweza kuikuza mara mbili ndani ya miezi sita mpaka mwaka bila ya kuhitaji usimamizi wangu wa karibu.
Mpaka huwa nacheka yani.
Sasa basi, kwa swali la aina hiyo ambalo ndiyo wengi huwa wanaanza nalo, haishangazi kwa nini wanahangaika sana na bado hawapati wanachotaka.
Kwa sababu kila kitu kina uwezo wa kumwingizia mtu yeyote yule fedha nyingi.
Lakini kila kitu kina vikwazo na changamoto zake na kinahitaji muda.
Kwa kuwa mtu anataka kwa haraka, anaona anachelewa, hivyo anaacha na kwenda kwenye kitu kingine.
Na hivyo ndivyo anajikuta amefanya vitu 10 ndani ya miaka 10 na hajapata fedha au utajiri aliokuwa anataka.
Mtu wa aina hiyo siyo kwamba hajui anachotaka au hajui anachopaswa kufanya, bali ni mpangilio usio sahihi.
Kutanguliza mkokoteni mbele ya punda.
Ambacho mtu anatakiwa kufanya, na ndiyo ambacho wote waliofanikiwa wamefanya ni kufunga mkokoteni nyuma ya punda na kisha kumwongoza punda kwenye uelekeo sahihi.
Maana yake ni wanaanza kwa kuamua nini wanataka kufanya, ambacho wapo tayari kukifanya kwa maisha yao yote hata kama hakuna anayewalipa.
Wakishaamua kile ambacho wapo tayari kukifanya, ndipo sasa wanajiuliza wanawezaje kulipwa kupitia kitu hicho.
Sijui unaona utofauti hapo rafiki yangu?
Wanaanza na wanachotaka kufanya, kisha wanaangalia namna ya kulipwa kupitia kufanya kitu hicho.
Maana yake ni wataendelea kufanya kitu hicho kwa muda mrefu, hata kama wanapitia magumu ambayo yanapelekea wasipate fedha kwa muda, hasa mwanzoni.
Kwa kufanya kwa muda mrefu, wanajiweka kwenye nafasi ya kuingiza fedha nyingi kwa baadaye.
Rafiki, fursa za kutengeneza fedha na utajiri ni nyingi mno, na zote zinafanya kazi.
Ikiwa utaanza na fedha kisha kutafuta fursa, utazimaliza zote na hutaupata utajiri.
Lakini kama utaanza na fursa kisha kujiboresha kiasi cha kuaminika, utapata utajiri mkubwa.
Anza kwa kuchagua nini unachotaka kufanya.
Chagua unataka kujulikana kwa kitu gani.
Chagua ni ujuzi wa aina gani unaotaka kuwa nao.
Halafu sasa, lipa bili yako.
Bili unayotakiwa kulipa ni ya kujenga huo ujuzi na uzoefu mkubwa.
Unavijenga hivyo kwa kujifunza na kufanya.
Kwa muda mrefu.
Bila shaka utapitia mengi sana wakati wa kujifunza na kufanya.
Utakosea sana.
Utapoteza sana.
Lakini kama hutakata tamaa na kuishia njiani.
Kama hutachoka haraka na kuacha.
Na kama utaendelea kufanya bila ya kuacha.
Ushindi ni wako.
Lazima utapata kile unachotaka.
Kwa sababu ndivyo wote unaowaona wamepata, walifanya.
Haitakuwa tofauti kwako.
Na hapo kwenye totauti ndiyo panahitaji tahadhari sana.
Maana ni rahisi kujihadaa kwamba itakuwa tofauti kwako.
Kwamba wewe huhitaji muda mrefu kama ambao wengine wamelazimika kupita.
Lakini huwezi kuizidi asili ujanja kwa muda mrefu.
Ukiweka mkokoteni mbele ya punda, utamchapa sana punda, lakini mzigo hautaenda mahali.
Utabadili hata punda, lakini kama bado unaweka mkokoteni mbele yake, hakuna mahali unaenda.
Shtuka, funga mkokoteni nyuma ya punda na mweke punda huyo kwenye uelekeo sahihi.
Ni swala la muda tu, ila kwa hakika utafika unakotaka kufika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Asante kocha.Kumbe ni muhimu kuhakikisha kuwa mkokoteni upo nyuma ya punda ili mzigo uweze kufika.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Funga mkokoteni nyuma ya punda na mweke punda huyo kwenye uelekeo sahihi.
Ni swala la muda tu ila kwa uhakika utafika unakotaka kufika.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Asante sana Kocha. Ninaenda KUFUNGA mkokoteni nyuma ya punda
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Nitafunga mkokoteni nyuma ya punda na sio mbele ya punda. Nakwenda kupiga hatua kumwa.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Asante Kocha,
Nikiufunga mkokoteni nyuma ya punda na kumwongoza kwenye njia sahihi, kukamilisha safari yangu salama ni swala la muda tu.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Ni kweli tufunge punda mbele mkokoteni nyuma na mjeredi mpya kazi iendelee
LikeLike
Kazi iendelee kwa uhakika.
LikeLike
Kustick na kitu kimoja kufanya kwa msimamo bila kuacha kulipa garama ili ujulikane kwa kitu kimoja na kupata matokeo makubwa
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Shtuka, funga mkokoteni nyuma ya punda na mweke punda huyo kwenye uelekeo sahihi.
Ni swala la muda tu, ila kwa hakika utafika unakotaka kufika.
LikeLike
Ndiyo.
LikeLike
Nitafika safari yangu kwa uhakika kabisa kwa kufunga mkokoteni nyuma ya punda na kisha kumwongoza punda kwenye uelekeo sahihi.Asante sana Kocha.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Chochote chenye mafanikio makubwa kinataka muda na kazi
Asante sana
LikeLike
Hayo mawili hayakwepeki.
LikeLike
Asante sana kocha kwa Makal bora sana kila kizuri kinahitaji muda
LikeLike
Karibu
LikeLike
Ni kweli kabisa!
Nimeamua kufunga mkokoteni nyuma ya Punda kwa kuamua nini cha kufanya na kukifanya kwa maisha yangu yote!
LikeLike
Safi sana.
LikeLike
Asante sana kocha, hakika ni kwenda kufunga mkokoteni nyuma ya punda na kumweka kwenye uelekeo wa kwenda.mabadiliko na umakini ni muhimu
LikeLike
Safi.
LikeLike