3211; Ukiacha kukwepa.

Rafiki yangu mpendwa,
Ni jambo la kushangaza, lakini kuna mambo unayojua unapaswa uyafanye, lakini umekuwa unayakwepa.
Mambo hayo ndiyo yenye nguvu ya kukufikisha kule unakotaka kufika.

Na katika mambo mengi unayopaswa kuyafanya, kuna moja muhimu sana ambalo lina nguvu ya kuleta matokeo makubwa na ya tofauti.
Hilo nalo umekuwa hulipi kipaumbele cha kutosha, kwani unahangaika na mengi na kushindwa kuweka muda na nguvu za kutosha kwenye hilo.

Biashara yako kuu unayofanya ndiyo unapaswa kuipa kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako.
Katika mengi ambayo unayafanya kwenye kila siku yako, kujenga biashara yako kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza.

Ndani ya biashara pia kuna mambo mengi ya kufanya, ambayo umuhimu wake unatofautiana.
Kwenye kila hatua ya biashara, jambo muhimu moja ambalo lina nguvu kuliko yote.
Kwenye ngazi ya chini kabisa, mauzo ndiyo jambo namba moja.
Kwenye ngazi ya kati, ubunifu kwenye kile kinachouzwa ndiyo jambo namba moja.
Kwenye ngazi ya juu, kuajiri watu wenye uwezo mkubwa wa kuiendesha biashara bila hata ya wewe kuwepo ndiyo jambo namba moja.

Umekuwa ukitawanya sana nguvu zako kwenye mambo mengi na kuishia kupata matokeo ya kawaida kwenye mambo hayo mengi.
Kama ungekusanya nguvu hizo kwenye jambo moja kwa wakati, kwa kipindi fulani, matokeo ambayo ungeyapata yangekuwa makubwa sana.

Kama kwa miaka 10 iliyopita, ambayo kila siku umekuwa unajishughulisha, ungeweka umakini na juhudi zako kwenye kuijenga biashara yako kuu pekee, leo hii ungekuwa mbali zaidi ya hapo ulipo sasa.
Badala yake uliruhusu baadhi ya mambo kukusumbua na hatimaye kuishia kupata matokeo makubwa.

Kadhalika kwenye biashara, kama kwa miaka hiyo 10 iliyopita ungeweka juhudi kwenye umakini na juhudi zako kwenye jambo moja muhimu kwa wakati, ungekuwa umekuza sana biashara.
Badala yake uligawa rasilimali zako kwa usawa na ukaishia kupata matokeo ya kawaida.

Hiki tunachokumbushana hapa, ni kanuni ya asili, ambayo inafanya kazi mara zote bila kushindwa.
Lakini bado kuna namna tunakuwa na wasiwasi na kushindwa kuweka imani yetu yote kwenye kanuni hizi.
Wasiwasi tunaokuwa nao unatupeleka kwenye mengi ambayo hayana tija kabisa.

Huwa tunakimbilia kufanya mambo ambayo yanatupa utulivu wa nafsi na kutuacha kwenye ukanda wetu wa faraja (Comfort Zone) kuliko yale ambayo yanaweza kutupa ukuaji zaidi.

Mara zote ukuaji wetu mkubwa huwa upo kwenye yale mambo ambayo tunakwepa kuyafanya, ambayo tunajua kabisa kwamba tunapaswa tuyafanye.

Tukiweza kuvuka hili la kukaa kwenye ukanda wa faraja, tukajisukuma kufanya yale tunayojua tunapaswa kufanya ila tunayakwepa, tutapiga hatua kubwa sana.

Wacha nikurudishe kidogo kwenye kanuni ambayo tumekuwa tunaijadili kwa miaka yote ambayo tumekuwa pamoja hapa.
Kanuni hiyo ni ya Pareto, au kwa jina jingine inaitwa kanuni ya 20/80.
Ambayo inasema asilimia 20 ya mambo unayofanya inazalisha asilimia 80 ya matokeo unayopata.
Kwa lugha nyingine kati ya mambo mengi unayoyafanya, kuna machache sana ambayo ndiyo yanachangia sehemu kubwa ya matokeo yanayopatikana.

Wengi huwa wanaelewa kanuni hii na kuifanyia kazi, ila kwenye ngazi ya kwanza na wanapata matokeo ya tofauti.
Lakini ili kupata matokeo makubwa kabisa, ambayo ndiyo yatakamilisha ndoto kubwa sana ulizonazo, unahitaji kwenda ngazi ya pili na ya tatu ya kanuni hii ya 20/80.

Twende kwa mfano ili tuelewane vizuri.
Kama kuna mambo 100 unayopaswa kufanya, 20 yanaleta matokeo makubwa kuliko 80. Kufanya hayo 20 na kuachana na 80 ndiyo ngazi ya kwanza ya kanuni ya 20/80.
Lakini katika hayo 20, kanuni bado inafanya kazi, kuna 4 ambayo yana matokeo makubwa kuliko 16 mengine.
Hivyo kwenye ngazi ya pili ya kanuni, mambo 4 yana matokeo makubwa kuliko 96. Unapaswa kufanya hayo manne.
Bado pia kanuni ina nguvu, kwenye mambo 4, kuna moja ambalo lina nguvu kubwa kuliko 3 mengine.
Hiyo ndiyo ngazi ya tatu ya kanuni ya 20/80, ambapo kwenye mambo 100 unayopaswa kufanya, kuna 1 ambalo lina nguvu kubwa kuliko 99 yanayobaki.

Swali ni hilo 1 ni lipi?
Hili ni swali ambalo hakuna mtu mwingine anayeweza kulijibu isipokuwa wewe pekee.
Kwa sababu halihusishi tu ukubwa au umuhimu wa kile kinachofanyika, bali pia inahusisha uwezo wako wa kipekee kwenye kufanya.

Hivyo basi, kanuni ya 20/80 usiwe tu unaishia kwenye ngazi ya kwanza, bali nenda mpaka ngazi ya tatu ili uweze kuelekeza nguvu zako kwenye eneo sahihi na ulete mapinduzi makubwa.
Ifikishe kanuni kwenye 1/99 na utaleta mapinduzi makubwa mno.

Rafiki, kuna miaka 10 ambayo ulishaipoteza huko nyuma kwa mahangaiko mengi yasiyokuwa na tija.
Itumie hiyo kama sehemu ya kujifunza.
Halafu sasa, kwa miaka 10 iliyo mbele yako kwa sasa, siyo ya kurudia makosa, bali ya kufanya kwa uhakika yale ambayo yatazalisha matokeo makubwa.

Nikuache na changamoto hii moja; hebu jaribu kuweka umakini na juhudi zako kubwa kwenye kitu kimoja kwa kukifanya kila siku bila kuacha na kwa muda mrefu halafu uone ni matokeo ya aina gani utayapata.
Huhitaji hata kujua ni jinsi gani itafanya kazi, wewe kuwa tu na imani na huu mchakato kisha fanya.
Matokeo utakayoyapata yatakushangaza sana.

Toka nje ya ukanda wako wa faraja kwa kujilazimisha kufanya yale ambayo umekuwa unayakwepa na utapata ukuaji mkubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe