3213; Aibu.

Rafiki yangu mpendwa,
Bilionea Peter Thiel amewahi kunukuliwa akisema watu wengi walioweza kuanzisha makampuni yaliyoleta mapinduzi makubwa hapa duniani, walikuwa na ugonjwa fulani wa akili ambapo hawajali wengine wanawachukuliaje.
Pale watu hao wanapoamua kitu cha kufanya, wanakifanya kama walivyopanga bila ya kukubali kukwamishwa na kitu chochote.

Katika kulijadili hilo, swali kuu la Thiel lilikuwa ni watu wasio na huo ugonjwa wanawezaje kusaidiwa nao wakaweza kufanya makubwa.
Na jibu lipo wazi, moja ya nguvu kubwa inayomwezesha mtu kufanya makubwa ni kutokuwa na aibu.
Aibu imekuwa kikwazo kikubwa sana kwa watu wengi kufanya kile walichopanga kufanya na kupata mafanikio makubwa.

Watu wengi ambao hawajapata mafanikio makubwa, siyo kwa sababu hawataki mafanikio au hawawezi kuyafanyia kazi.
Bali ni kwa sababu ya aibu.
Pale wanapohitajika kufanya vitu ambavyo ni tofauti na mazoea yao au wengine wanapowashangaa kwa wanayofanya, wanaacha kufanya.

Watu wengi huwa wanatengeneza magereza ya maisha yao, kisha kukaa huko kwa maisha yao yote.
Hawathubutu kutoka kwenye magereza hayo ya kujitengenezea wao wenyewe.
Na sababu kuu ni aibu.

Watu wamekuwa wanajali sana wengine wanawafikiria na kuwachukuliaje kuliko wanavyojali nini wanapaswa kufanya ili kupata wanachotaka.

Sasa basi, inatulazimu kuigiza ugonjwa wa wale walioweza kufanya makubwa kwa kutokujali sana wengine wanawachukuliaje.
Tunahitaji ‘kujichetua’, kujitoa ufahaku na kujizima ‘data’.

Tunachopaswa kuangalia ni nini kinachopaswa kufanya na kukifanya na siyo nini wengine wanatutegemea tufanye.

Kwenye safari yetu ya kujenga Ubilionea, hiyo inamaanisha hakuna kazi yoyote ambayo ni ya chini ya viwango vyako au siyo hadhi yako.
Kama kitu ni sahihi na kinakuingizia fedha, unapaswa kukifanya kwa ukubwa bila kujali wengine wanakuchukuliaje au kusemaje.

Pia usione aibu unajifunza kwa nani.
Kama umekutana na nafasi ya kujifunza, jifunze bila ya kuona aibu unajifunza kwa nani.
Wengi huwa wanaona aibu kujifunza, hasa kwa watu walio chini yao na kuishia kubaki na ujinga wao.
Wewe usiwe hivyo, tumia kila fursa kujifunza kutoka kwa kila mtu.
Hata watoto wadogo au watu unaowaona ni wa hovyo, wana mengi sana ya kujifundisha.

Kwa kifupi aibu ni kikwazo kikubwa sana kati yako na mafanikio makubwa unayoyataka.
Kadiri unavyokuwa na aibu kwenye mengi unayopaswa kufanya, ndivyo unavyojichelewesha kupiga hatua.

Kuanzia sasa, tuufanyie kazi huo mshipa wa aibu.
Tayari tunajua tunachotaka na tunajua tunachopaswa kufanya ili kukipata.
Wajibu wetu ni kufanya kila tunachopaswa.
Hatupaswi kujali wengine wanatufikiria au kutuchukuliaje.
Pale mshipa wa aibu unaposimama, tunapaswa kuukalisha chini.
Tunapaswa kubadili tafsiri yetu kwenye aibu, kwa kujipa sababu ya kufanya yale yote tunayoyaonea aibu kufanya.

Na kama kuna mtu amefanikiwa kuliko wewe na kuna mambo anayofanya ambayo yamechangia mafanikio yake, ila wewe unajiambia huwezi kuyafanya hayo, hiyo ni sababu kwa nini mtu huyo amefanikiwa kukuzidi.

Haimaanishi kwamba ukifanya yale yanayofanywa na wengine basi utapata mafanikio kama yao.
La hasha, muhimu ni unapaswa kufanya yale unayojua kabisa unatakiwa kuyafanya, lakini aibu inakukwamisha.
Fanya yote sahihi ambayo umekuwa unayaonea aibu kuyafanya na utaweza kupiga hatua kubwa sana.

P.T. Barnum, aliyekuwa mfanya maonyesho maarufu na aliyetumia sana njia ya ‘kiki’ kujaza watu kwenye maonyesho yake amewahi kunukuliwa akisema: “Sijali magazeti yanasema nini kuhusu mimi, muhimu tu ni waandike jina langu kwa usahihi.”
Hii ni ngazi ya juu kabisa ya kuondokana na aibu na kufanya unachopaswa kufanya.

Bilionea mwingine ambaye alikuwa maarufu kwa kuwekeza kwenye makampuni kisha kuyateka pale alipokuwa haridhishwi na uongozi iliopo, watu walikuwa wanamwambia anasemwa vibaya kwamba ni mtu mwenye roho mbaya na asiyejali.
Na yeye jibu lake lilikuwa; “Sijali sana watu wananiita nani, wasiniite tu kuku halafu wakanila nyama.

Haijalishi unafanya nini kwenye maisha yako, hutaweza kumridhisha kila mtu na watu hawataacha kusema.
Hivyo weka aibu pembeni na ufanye yale unayopaswa kufanya ili kupata unachotaka kupata.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe