3217; Nyenzo ya juu kabisa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuanza biashara na kuikuza ni vitu viwili tofauti kabisa.
Hapo ndipo watu wengi sana wanapokwama kwenye safari zao za kibiashara.

Wengi wanapoanza biashara huwa wanakuwa wapo peke yao na hivyo kila kitu kufanya wao.
Wanapokuwa wanashindwa kufanya kitu, wanaona ni kitu ambacho hakiwezi kufanyika kibiashara.

Wanasahau kwamba uwezo wao binafsi na uwezo wa biashara ni vitu tofauti kabisa.
Uwezo binafsi wa mtu unaweza kuwa na ukomo mbalimbali kulingana na mtazamo ambao mtu anakuwa nao.
Lakini uwezo wa biashara hauwezi kuwa na mwisho kama biashara imeachwa huru ikue.

Hivyo wajibu namba moja wa kila mfanyabiashara ni kuhakikisha vikwazo vyake binafsi haviwi vikwazo vya ukuaji wa biashara yenyewe.

Kuna ngazi tatu za mrejesho pale inapohitajika kufanya kitu cha tofauti kwenye biashara.

Ngazi ya chini kabisa ni “hicho hakiwezekani”.
Kwa sababu mtu anaona hawezi kufanya kitu, basi moja kwa moja anachukulia biashara haiwezi kufanya.
Hiki ndiyo kimekuwa chanzo cha kifo cha biashara nyingi.

Ngazi ya kati ni “kinawezekanaje?”
Hapa mtu anauliza ni kwa namna gani kitu kinaweza kufanyika.
Lakini hapo anakuwa anajiuliza kwake yeye mwenyewe.
Hapa ndipo biashara nyingi zinapodumaa na kushindwa kukua, kwa sababu mmiliki wa biashara anataka kufanya kila kitu yeye peke yake.

Ngazi ya juu ni “nani anaweza kukifanyia kazi?”
Hapa mtu anauliza ni watu gani ambao wanaweza kukifanyia kazi kile kinachohitajika kufanywa.
Hapa ndipo penye ukuaji mkubwa wa biashara na usiokuwa na ukomo.
Kwa sababu biashara haimtegemei mwanzilishi pekee.

Nyenzo ya juu kabisa kwenye biashara huwa ni NANI na siyo nini au vipi.
Unapoweza kuwapata watu wengi sahihi wa kutekeleza yale yote yanayopaswa kutekelezwa kwenye biashara, ukuaji unakuwa wa uhakika.

Watu wanaongeza muda zaidi kwenye biashara, hivyo kadiri watu wanavyokuwa wengi ndivyo kikwazo cha muda kinavyopungua.
Watu pia wanaongeza ujuzi na uzoefu muhimu unaohitajika sana kwenye ukuaji wa biashara.

Kwa sababu hii basi, unapaswa kufanya mabadiliko makubwa ya kimtazamo kwenye biashara.
Hama kutoka kufikiria NINI na VIPI na nenda kwenye kufikiria NANI.
Kwa kila kinachopaswa kufanyika kwenye biashara, usiangalie kwa nini hakiwezekani au wewe huwezi kufanya.
Bali angalia nani anayeweza kukifanya kwa usahihi.

Kwa kuwa watu ndiyo nyenzo ya juu kabisa, unapoweza kuifanyia kazi, unaondoa vikwazo vyote vya ukuaji wa biashara yako.
Weka nguvu zako zote hapo na utaweza kufanya makubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe