3220; Unayasababisha mwenyewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo mengi yanayokuvuruga na yanayokuwa kikwazo kwako kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Unaweza kuona wengine ndiyo wanaosababisha mambo hayo, lakini kiuhalisia, wewe ndiye umekuwa unayasababisha mwenyewe.

Kuna nyakati unapatwa na hasira sana kwenye maisha yako, ambazo zinapelekea ufanye maamuzi yasiyokuwa sahihi. Unaweza kuona hasira hizo zimesababishwa na wengine, kutokana na yale waliyofanya au kushindwa kufanya.
Lakini ukweli ni hasira hizo ni zako mwenyewe, ambapo umezisababisha kwa kuwa na matarajio makubwa kwa watu wengine. Pale watu wanapoenda tofauti na matarajio unayokuwa nayo, ndiyo unapatwa na hasira.
Hivyo basi, ili kuondokana na hasira, acha kuwa na matarajio makubwa kwa watu wengine. Pokea na kubali yale watu wanatoa na kazana na yale unayoweza kuyadhibiti wewe mwenyewe.

Unaweka juhudi kubwa sana kwenye kile unachofanya, lakini bado umekwama, huoni ukipiga hatua ambazo ulitarajia uwe umepiga.
Kwenye hali kama hii unaweza kuona kama kuna watu wanakukwamisha au mambo fulani yanayokuwa kikwazo kwako.
Lakini ukweli ni mkwamo unatokana na usumbufu. Ni pale unapohangaika na mambo mengi ndiyo juhudi zako zinapotea huku ukishindwa kupiga hatua ulizotaka kupiga.
Kama kweli unataka kupiga hatua kubwa, achana na usumbufu wote unaohangaika nao.
Na hapa usumbufu ni chochote ambacho hakina mchango kwako kufika kule unakotaka kufika.
Fokasi kwenye kitu kimoja mpaka kikupe mafanikio makubwa ndiyo uende kwenye kitu kingine.

Kuna nyakati unapatwa na wasiwasi mkubwa kwenye kile unachokitaka. Wasiwasi unakuwa ni kama unaweza kukipata au la.
Unaweza kuona wasiwasi huo unatokana na ugumu wa kupatikana kwa kile unachotaka.
Lakini huo siyo ukweli, wasiwasi unaokuwa nao unatokana na wewe kuwa na muda mwingi ambao huna cha kufanya.
Kadiri unavyokuwa na muda mwingi wa bure, ndivyo wasiwasi unavyopata nafasi ya kutawala akili yako na kukusumbua.
Hivyo unachopaswa kufanya ni kuhakikisha muda wako wote umeupangilia kwa mambo muhimu ya kufanya.
Usikubali kuwa na muda ambao huna kitu cha kufanya, pangilia kila dakika yako kwa mambo ambayo ni lazima uyafanye na utajikuta huna nafasi ya kuwa na wasiwasi.

Kuna vitu vingine vimekuwa vinakukwamisha na unadhani vinasababishwa na wengine kumbe ni wewe mwenyewe.
Unapijiona mpweke, unaweza kudhani ni kwa sababu hakuna watu wengine wanaokuthamini na kukukubali.
Lakini ukweli ni upweke huwa unaanza na wewe mwenyewe, pale unaposhindwa kujithamini na kujikubali.
Upweke ni kushindwa kuwepo kwa ajili yako mwenyewe.

Unapopatwa na uchovu unaweza kuona ni kazi kubwa na nyingi unazofanya.
Lakini hilo siyo kweli, uchovu unatokana na kuyapoteza maisha yako kwa ajili ya wengine.
Pale unapofanya mambo kwa ajili ya wengine, iwe ni kwa kuiga au kutaka kuwaridhisha, ndiyo unapatwa na uchovu mkubwa.
Lakini unapofanya mambo kwa ajili yako mwenyewe, yale ambayo ni ya muhimu kabisa kwako, huwezi kuchoka.

Jambo la mwisho ni upotevu wa maisha kwa ujumla. Wengi huja kushtuka miaka imeenda na hakuna makubwa ambayo wameyafanya.
Tatizo kubwa linakuwa ni mtu kukimbizana na raha muda wote.
Kwa kuhangaika na raha, wanajikuta wakiendekeza vitu ambavyo havina manufaa ya muda mrefu kwao na hivyo kujikuta wakiyapoteza maisha yao.

Jenga maisha yako kwa kuwa na maono na ndoto kubwa kisha kuzipambania.
Jua yale unayopaswa kufanya ili kupata unachotaka kupata, kisha fanya hayo tu na usiruhusu usumbufu wowote ukuingilie.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe