3233; Usiseme, onyesha.

Rafiki yangu mpendwa,
Hii dunia haijawahi kuishiwa wasemaji.
Kila mtu anaweza kusema, kwa kupanga na kuahidi mambo mengi.
Lakini inapokuja kwenye ufanyaji, kuna uhaba mkubwa wa watu.
Ni watu wachache sana ambao ni wafanyaji kweli kwenye kile wanachotaka.

Kila mtu anataka mafanikio makubwa na utajiri.
Kila mtu anataka kuwa na maisha mazuri.
Lakini hi wachache sana ambao wanapata vitu hivyo.
Siyo kwa sababu hao wachache wamependelewa au wana bahati kuliko wengine.
Bali ni kwa sababu hao wachache ndiyo wapo tayari kutoka nje ya mazoea yao na kufanya vitu vipya na vikubwa.

Kama na wewe unataka kuwa sehemu ya hao wachache ambao wanapata kile wanachotaka, unachopaswa kufanya ni kuacha kusema na kuanza kuongesha.
Unapaswa kuacha maneno na kuweka kazi.
Chukua hatua kubwa na za tofauti.
Fanya vitu ambavyo hujawahi kufanya.
Nenda nje ya mazoea yako.

Wala siyo kwamba watu ni wavivu kihivyo.
Kinachowazuia kuchukua hatua siyo uvivu.
Bali ni ile hofu ya kushindwa au kupoteza pale mtu anapofanya kitu kipya na ambacho hajazoea.

Hivyo kinachohitajika hapa ni kubadili mtazamo.
Kwa sababu kinachofanya mtu ashindwe siyo kufanya na kushindwa, bali kutokufanya kabisa.
Ukifanya na kushindwa unakuwa umejifunza, hivyo wakati mwingine utafanya kwa ubora zaidi.
Lakini usipofanya, hakuna unachojifunza.

Kuna ambao huwa wanapata msukumo wa kuchukua hatua kubwa.
Na mwanzoni wanachukua hizo hatua kweli kweli.
Lakini hawapati matokeo waliyokuwa wanategemea kuyapata.
Na hilo linawapelekea kukata tamaa na kuacha.
Hiyo ni changamoto nyingine inayowakwamisha wengi.

Hutafanikiwa kwa kufanya mara chache au pale unapojisikia kufanya.
Bali utafanikiwa kwa kufanya kila mara, kwa msimamo bila kuacha.
Ni ule msimamo wa kufanya ndiyo wenye nguvu kuliko hata ukubwa wa ufanyaji wenyewe.
Kama huwezi kufanya kitu kwa msimamo na kwa muda mrefu bila kuacha, jua dhahiri kabisa kwamba hutaweza kupata matokeo makubwa unayotaka kuyapata.

Kinachopelekea ndoto za wengi kufa siyo kwa sababu haziwezekani.
Bali ni kwa sababu hawazipi ndoto hizo juhudi za kutosha.
Kuota pekee hakuna nguvu kubwa, kila mtu ana ndoto nyingi na kubwa.
Ni kuchukua hatua ndipo mafanikio yalipo.
Kufanya ndiyo kunazileta ndoto kwenye uhalisia.

Hivyo basi, unapokuwa na ndoto, unaweza kuchagua kuendelea kulala ili kufurahia ndoto hizo ila maisha yako halisi yakabaki vile vile.
Au unaweza kuamka na kwenda kuchukua hatua kwenye ndoto ulizonazo na ukaweza kuzileta kwenye uhalisia.
Pale ndoto zinaposhindwa, matendo huwa yanafanikiwa, mara zote.

Usiwe tu mtu wa kusema, onyesha kwa kufanya na hivyo ndivyo unavyoleta mabadiliko ya kweli na yanayokupa mafanikio unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe