💯KCM2324009; Umewafundisha.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.

Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

Jipatie nakala yako leo, piga simu 0752977170



💯 Neno la leo; Umewafundisha

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaangalia jinsi ambavyo wewe mwenyewe unawafundisha watu jinsi ya kukuchukulia.

Jinsi ambavyo watu wanakuchukulia wewe, ni wewe mwenyewe umewafundisha.
Watu huwa wanakuchukulia jinsi unavyojichukulia wewe mwenyewe.

Kama unajipenda wewe mwenyewe, watu pia watakupenda.
Kama unajiamini wewe mwenyewe, watu pia watakuamini.
Hakuna watu wanaokufanyia kinyume na vile unavyojifanyia wewe mwenyewe.

Kwenye maisha huwa hatupati kile tunachostahili, bali tunapata kile tunachokipambania.
Hupati kile unachotaka kupokea, bali unapata kile unachokataa kupoteza.

Kile unachojifanyia wewe mwenyewe, utawavumilia wengine wanapokufanyia.
Kama unajidharau, wengine wakikudharau utawavumilia, maana siyo kitu kipya kwako.
Na hapo kila mtu atakudharau.

Kujikubali ni hatua muhimu ya kuachilia breki kwenye maisha yako na kukuwezesha kupata kile unachotaka.
Unapojikubali sana wewe mwenyewe, hutaweza kuwavumilia wale ambao hawakukubali.
Hivyo matokeo yake ni kukubalika na wengine na kiweza kupata yale unayotaka.

Pale unapoona wengine wanakufanyia mambo ambayo hutaki wakufanyie, jiulize ni kwa namna gani umewafundisha wawe wanakufanyia hivyo.
Kwa sababu ni wewe umewaruhusu wafanye hivyo.
Hakuna mwenye uthubutu wa kukufanyia kitu ambacho wewe mwenyewe hukubaliani nacho.

Waonyeshe watu vile unavyotaka wakuchukulie.
Jipende na jikubali wewe mwenyewe na usimvumilie yeyote ambaye hakupi vile ambavyo unajipa mwenyewe.
Kwa njia hiyo utapeleka ujumbe kwa wengine wanapaswa kukuchukuliaje.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kutokufanya bali kuonyesha. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/07/3233

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku unayokwenda kushika hatamu ya maisha yako na kuifanya kuwa ya kipekee kabisa kwako.

Kocha.
💯