3235; Wape kile wanachotaka.

Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja kikubwa sana ambacho naendelea kujifunza kwenye biashara ni kwamba ukitumia akili nyingi sana, unaishia kushindwa.

Yaani kadiri unavyokazana kuchambua na kupangilia biashara kwa akili kubwa, ndivyo unavyozidi kuipoteza na hata kupelekea ife.

Kanuni kuu ya mafanikio kwenye maisha ni kupata unachotaka, wape wengine kile wanachotaka.
Kanuni hiyo pia inafanya kazi kwenye biashara.
Ili uweze kufanikiwa kwenye biashara, unapaswa kuwapa watu kile wanachotaka.

Wape kile ambacho tayari wanakitaka na siyo unachodhani wanatakitaka.
Kuwapa watu kile wanachotaka haihitaji akili kubwa sana.
Ni kuwasikiliza watu na kisha kuwapa kile wanachotaka.
Kuwapa watu kile unachodhani wanakitaka inahitaji akili kubwa sana, na bado utashindwa.

Yapo mazoea ya watu kujipima na vitu mbalimbali kwenye biashara zao, vitu ambavyo mteja hana muda navyo kabisa.
Tukumbushane kwamba watu hawanunui kwa sababu tunauza.
Bali wananunua kwa sababu zao binafsi, pale wanapokuwa na uhitaji na wanapoona wanapata thamani kubwa kulinganisha na gharama wanazolipa.

Tukizidi kurahisisha kanuni hiyo ya mafanikio kwenye biashara tunakuja na hii rahisi zaidi kueleweka na kutekeleza; Toa Thamani Kubwa = Kulipwa vizuri.

Wateja hawalipi kwa kigezo cha kuweza kumudu au la. Bali wanalipa kwa kigezo cha thamani kubwa wanayoipata ukilinganisha na gharama wanayopaswa kulipa.

Hiyo ina maana kwamba kama mteja ataona fursa ya kupata thamani kubwa, atajisukuma kwa kila namna huhakikisha anaweza kumudu kitu hicho.

Kazi yako kubwa ni kuhakikisha unatoa thamani kubwa sana kwa wateja wako, kwa kuwapa kile wanachotaka, kwa namna ambayo hawawezi kupata mahali pengine.

Akili yoyote kubwa utakayotumia kwenye biashara na isiguse kuwapa watu kile wanachotaka na kwa thamani kubwa ni upotevu.
Utahangaika sana, lakini mahangaiko hayo hayataleta matunda.

Nasisitiza hili ili likuondoe kwenye matamanio ya kutaka kutumia akili nyingi kwenye biashara na ukaishia kushindwa; wateja hawanunui kwa sababu unauza, bali kwa sababu wana mahitaji yao binafsi.

Watu hawajali sana umefanya kazi masaa mangapi.
Hawajali umeingia gharama kiasi gani.
Wala hawajali wewe binafsi una mahitaji kiasi gani.
Wao wanachoangalia ni wananufaikaje, wanapataje kile wanachotaka.
Ukiweza kuwapa watu kile wanachotaka, kwa thamani kubwa ambayo hawawezi kuipata mahali pengine, una ushindi mkubwa kwenye mauzo.

Kila unapojikuta unataka kutumia akili kubwa kwenye biashara, jiulize kama tayari unatimiza yale ya msingi kabisa ambayo ni kuwapa watu kile wanachotaka kwa thamani kubwa.

Viungo viwili ambavyo vitakusaidia sana kwenye biashara ni macho na masikio.
Macho yako yanapaswa kuwa kwenye kuziangalia namba za biashara yako, kujua mwenendo wake kila wakati.
Masikio yako yanapaswa kuwa yanawasikiliza wateja wa biashara kwa yale wanayosema.

Wasikilize watu, kisha wape kile wanachotaka. Huhitaji akili kubwa zaidi ya hiyo ili kufanikiwa kwenye biashara.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe