💯KCM2324016; Mpaka.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.

Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

Hii inaitwa biblia ya mafanikio, ni kitabu cha kusoma kila siku kwa mwaka mzima na chenye madini mengi sana. Jipatie nakala yako sasa, 0752 977 170.



💯 Neno la leo; Mpaka.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaangalia kujikubali na matumizi sahihi ya muda wako kufanya makubwa.

Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawashangaza watu ni jinsi ambavyo muda una usawa kwa watu wote.
Kwamba kila mtu ana masaa 24 pekee kwenye siku yake.

Lakini kwenye muda huo ambao uko sawa kwa watu wote, matumizi yake yamekuwa hayafanani wala kulingana.
Kuna ambao wanatumia muda huo kufanya makubwa na kufanikiwa.
Na kuna ambao wanapoteza muda huo kwa kufanya mambo ya hovyo na kushindwa.

Wengi huhangaika na muda, wakidhani labda tatizo linaanzia kwenye muda.
Lakini wamekuwa hawafanikiwi kulitatua hilo hata baada ya kukazana kulinda muda wao.
Bado wanajikuta wakiwa wanaupoteza na kushindwa kufanikiwa.

Ukweli ni kwamba tatizo limekuwa halianzii kwenye muda.
Bali tatizo linaanzia kwenye kujikubali na kujithamini.

Ni MPAKA pale mtu atakapojikubali na kujithamini binafsi ndiyo ataweza kuuthamini muda wake.
Na ni MPAKA pale unapothamini muda wako ndiyo unaweza kuutumia kufanya makubwa.

Hapo tunaona tatizo la muda linapoanzia, siyo kwenye kuwepo au kutokuwepo kwa muda. Bali kujikubali na kujithamini.

Wote wanaotumia muda wao vizuri na kufanikiwa wanajikubali na kujithamini sana.
Hilo linawafanya wathamini sana muda wao na kuutumia kufanya makubwa.
Na hilo ndiyo linalowafikisha kwenye mafanikio makubwa.

Na wale wanaotumia muda wao vibaya kwa kuupoteza kwenye mambo yasiyokuwa na tija, hawajikubali wala kujithamini.
Wanajiona ni watu wa kawaida ambao hakuna makubwa wanayoweza kufanya.
Hilo linawapelekea kupoteza muda wao kwenye mambo yasiyokuwa na tija, kitu kinachokuwa kikwazo kwa mafanikio yao.

Kabla hujahangaika na muda, hebu anza na thamani yako binafsi.
Kujikubali na kujithamini ni njia ya kuachilia breki ambazo zimekuwa zinawazuia watu kupata mafanikio makubwa.
Vile unavyojichukulia ndivyo wengine pia wanavyokuchukulia.
Vile unavyochukulia muda wako, ndivyo pia wengine wanavyouchukulia.
Anza kujikubali na kujithamini wewe mwenyewe na mengine yote yataenda vizuri.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ukuaji na changamoto. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/14/3240

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku unayokwenda kujikubali na kujithamini ili kutumia vizuri muda wako na kufanya makubwa.

Kocha.
💯