3244; Mara moja moja na kila mara.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha kuna mambo ambayo mtu unaweza kujikusanya na kuyafanya mara moja moja.
Yanaweza kuwa mambo makubwa na ya kishujaa, ambayo wengi hawawezi kuyafanya.

Lakini bado ni mambo ambayo hayawezi kumpa mtu mafanikio makubwa.
Hiyo ni kwa sababu mafanikio siyo zao la kufanya kitu mara moja moja, bali kufanya kila mara.

Ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote, lazima uweze kulifanya kila mara na kwa muda mrefu.
Kila unachofanya kinajikusanya na kuchangia mafanikio makubwa.

Sahau kuhusu kujikusanya na kuweza kufanya makubwa sana mara moja moja. Japo unaweza kufanya makubwa ndani ya muda mfupi, hayawezi kuchangia kwenye mafanikio makubwa na yanayodumu.

Unachopaswa kujenga ni uwezo wa kufanya kitu kila mara, kwa msimamo bila kuacha.
Hata kama unavyofanya ni vya kawaida, uwezo wa kufanya kila mara, unawezesha kuzalisha matokeo bora.

Ushujaa wa kuweza kufanya makubwa kwa muda mfupi unaweza kuwafurahisha watu.
Lakini mafanikio makubwa na yanayodumu ni zao yale unayofanya kila mara bila kuacha.

Kitu chochote ambacho utachagua kukifanya kila siku bila kuacha, hata kama hufanyi kwa ukubwa, mkusanyiko wa ufanyaji kwa kujirudia rudia una nguvu kubwa ya kuleta mafanikio.

Kwa maana hiyo basi, chochote unachopanga kuanza kufanya, jiulize kama unaweza kukifanya kila siku bila ya kuacha.
Kama jibu ni ndiyo, basi endelea kufanya, maana hapo kuna fursa ya kufanikiwa.
Lakini kama kuna chochote kinachoweza kukuzuia usifanye kila siku, basi hutaweza kufanya kila siku na hilo litakuzuia kupata mafanikio makubwa.

Kila mtu anaweza kujikusanya na kufanya jambo la kishujaa mara moja moja.
Lakini kufanya kila mara na kwa msimamo, hata kama ni vitu vya kawaida, wengi wanakwama.
Na pale wengi wanapokwama ndipo huwa na mafanikio makubwa.

Hivyo basi, kanuni ya mafanikio ni rahisi na imenyooka;
1. Chagua kile ambacho unaweza kukifanya kila mara bila kuacha.
2. Fanya kila mara hata pale unapokuwa na sababu ya kuacha kufanya.
3. Usihangaike sana na mambo magumu kabla hujafanya yale ya msingi kabisa.
Tukae humo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe