3248; Endelea na huo mpango.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa tunakuwa na malengo makubwa, ambayo tunayawekea mipango ya kuyatekeleza malengo hayo na kuyafikia.

Tukishaweka mipango huwa tunakuwa na shauku kubwa ya kuitekeleza, tukiona jinsi ilivyo rahisi na uhakika kufikia malengo hayo.
Yote hiyo ni mipango, ambayo bado tunakuwa hatujaanza utekelezaji wake.

Ni pale tunapoanza utekelezaji ndiyo mambo yanakuwa tofauti.
Matokeo tunayoyapata mwanzoni yanakuwa tofauti kabisa na matarajio tunayokuwa nayo.
Yaani matokeo yanakuwa ni mabaya sana ukilinganisha na matarajio ambayo tulikuwa na uhakika nayo.

Hapo ndipo watu wengi hukata tamaa na kuachana na mpango waliokuwa nao.
Wanaandaa mpango mwingine ambao wanaona utakuwa rahisi na wa uhakika zaidi kwao.
Lakini mambo yanajirudia hivyo hivyo hata kwenye mpango mwingine.

Ukweli ni kwamba hata upange vizuri kiasi gani, hata uwe na uhakika kiasi gani, mwanzo wa jambo lolote lile huwa ni mgumu na usiokuwa na uhakika.
Unaweza kufanya kama ulivyokuwa umepanga, lakini matokeo utakayoyapata yanakuwa ya tofauti kabisa na ulivyotegemea.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila anayejaribu kufanya makubwa.

Ni muhimu sana usikate tamaa pale matokeo unayoyapata yanapokuwa tofauti na mategemeo uliyokuwa nayo.
Badala yake unapaswa kuendelea na huo mpango kama ambavyo ulikuwa umeuweka.
Unachopaswa kufanya ni kwenda ukiboresha kulingana na matokeo unayoyapata.
Lakini kamwe usikate tamaa kwa matokeo mabaya ya mwanzoni.

Mwanzo huwa ni mgumu kwa kila mtu.
Ni kudumu kwa muda mrefu kwenye kitu ndiyo kunawapa watu mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka.

Hivyo wewe endelea kufanya, kama ulivyopanga, hatua kwa hatua na kwa muda mrefu zaidi bila kuacha.
Ukienda hivyo, haitachukua muda mrefu kabla hujaanza kupata matokeo mazuri, ya uhakika na kwa msimamo.

Matokeo hayo mazuri yanakuwa ni zao la kubaki kwenye kufanya kwa kuweza kuvuka ugumu na ukatishaji tamaa wa mwanzo.

Unayo malengo makubwa,
Ambayo umeyawekea mipango mizuri.
Na ukaanza kuitekeleza mipango hiyo kwa shauku kubwa.
Lakini matokeo unayopata mwanzo ni tofauti kabisa na matarajio.
Tafadhali sana usikatishwe tamaa haraka na hayo matokeo.
Badala yake endelea kufanya kama ulivyofanya.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa.
Hivyo ndivyo wewe utakavyofanikiwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe