3249; Maarifa pekee hayatoshi.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya mapingamizi ya watu wasiopenda kusoma vitabu ni kwamba hata waandishi na wauzaji wa vitabu hivyo hawajaweza kunufaika na kile kilichoandikwa kwenye vitabu hivyo.

Huwa kuna utani kwamba mtu aliandika kitabu cha jinsi ya kupata mtaji wa kuanza biashara. Lakini akashindwa kuchapa kitabu hicho kutokana na kukosa mtaji.

Wanachofikiri wengi ni kwamba ukishapata maarifa basi kimiujiza unabadilika kupitia maarifa hayo.
Hicho ni kitu ambacho hakina hata chembe ya ukweli.

Ni kweli maarifa ni muhimu ili mtu aweze kufanikiwa.
Lakini ni sehemu ndogo sana ya yale yanayohitajika ili kufanikiwa.
Ili maarifa yalete matunda, lazima yawekwe kwenye vitendo.
Ndiyo maana kanuni kuu ya KISIMA CHA MAARIFA NI MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.

Kupitia kanuni hiyo na hata uelewa wa mawaida, tunakubaliana kwamba maarifa pekee hayamtoshi mtu kufanikiwa.
Lazima mtu ayaweke maarifa hayo kwenye vitendo ndiyo yaweze kumpa matokeo mazuri.

Wengi kwa kusikia kinachohitajika ni kuweka maarifa kwenye vitendo ndiyo kunaleta mafanikio, wanakazana kufanya hivyo.
Lakini bado hawapati mafanikio wanayokuwa wanayataka.
Kinachokuwa kimetokea ni wengi kukata tamaa haraka kabla ya kupata mafanikio.
Wanapochukua hatua na kuona mafanikio waliyoyataka hayaji, wanakata tamaa na kuacha.

Ili mtu kuweza kuvuka hayo na kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake kupitia maarifa anayopata, anahitaji vitu viwili; Kocha na Uwajibikaji.

Kocha anakusimamia kwenye utekelezaji wa yale yote uliyojifunza.
Kocha hatakuachia ukate tamaa na kuacha pale mambo yanapokuwa magumu.
Badala yake atahakikisha unaendelea kuchukua hatua mpaka unapata matokeo unayokuwa unayata.

Uwajibikaji unafanya gharama ya kutokufanya kuwa kubwa kuliko ya kufanya.
Yaani inakuwa ina gharama kubwa kwako kama utaacha kufanya, kuliko ukifanya.
Hilo linakusukuma ufanye hata kama bado huoni matokeo.

Hivyo rafiki yangu mpendwa, kama unayataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unahitaji kuwa na Kocha ambaye atahakikisha unafanya bila ya kuruhusu sababu zozote zikukwamishe.
Pia unahitaji mfumo wa uwajibikaji ambao unakusukuma kufanya bila kuacha hata kama matokeo ni tofauti na ulivyopanga.

Vitu hivyo viwili vina nguvu kubwa ya kumwezesha mtu kufanya makubwa kwenye maisha yake.
Na kwa bahati nzuri sana, kama unasoma hapa, tayari unavyo vitu hivi.
Tayari unaye Kocha aliye tayari kukusimamia kuweka kwenye matendo yale unayojifunza.
Lakini pia upo mfumo wa uwajibikaji unaokulazimisha ufanye ili usiingie gharama kubwa.
Mfumo huo ni wa kuchukua hatua kidogo kidogo kwa kushirikisha kwa wengine.

Ukishapata maarifa, jipongeze maana hapo umekamilisha hatua moja kati ya hatua 100.
Hatua 99 zilizobaki ni za kuchukua hatua kwenye yale ambayo umejifunza.
Tekeleza hatua hizo 99 ili uweze kupata mafanikio unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe