3250; Tayari unalipa hiyo gharama.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye uzalishaji huwa kuna dhana kwamba kama kampuni inahitaji kupata zana fulani ambayo itaongeza uzalishaji, lakini ikawa haiwezi kumudu gharama za zana hiyo, tayari inakuwa inalipa hiyo gharama.
Hiyo ni kwa sababu kwa kampuni kukosa hiyo zana, inakuwa na uzalishaji mdogo na hivyo kukosa yale manufaa ambayo yangekuja na ongezeko la uzalishaji.

Kwa lugha rahisi ni kwamba kushindwa kulipa gharama ya kitu fulani ambacho kina manufaa, inakugharimu kwenye manufaa unayoyakosa.

Kama biashara yako ina uhitaji wa kuajiri mtu, lakini ukashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya gharama, jua hujakwepa gharama hiyo.
Unakuwa tayari unalipa hiyo gharama, kwa wewe kufanya mambo ambayo mwingine angeweza kuyafanya.
Hilo linakugharimu sana kwa upande wa muda, ambao unashindwa kuutumia kwa usahihi.
Na inapokuja kwenye muda, thamani yake huwa ni kubwa kuliko ya fedha.

Kwenye maisha, hakuna gharama ambazo mtu anaweza kuzikwepa.
Ni labda anaamua kulipa gharama hizo moja kwa moja na kupiga hatua.
Au mtu anakwepa kuzilipa kwa sababu anaona hawezi kuzimudu, kitu ambacho kinaendekea kumgharimu na kumkwamisha kupiga hatua.

Chochote unachoona unakihitaji ili kukua zaidi, lakini unakwama kwa sababu ni ghali kwako, jua tayari unalipa hiyo hiyo gharama kwa ukuaji unaoukosa.
Hivyo ni wewe uchague kulipa gharama na kupata matokeo.
Au uone gharama ni kubwa kuliko uwezo na uishie kulipa gharama kubwa zaidi.

Elewa vizuri hii dhana ya kulipa gharama kwenye kila eneo lako na mifano yako binafsi ya jinsi umekuwa unakwepa gharama hizo na kuwa umeishia kulipa gharama kubwa zaidi kwenye ukuaji unaokuwa umekosa.

Kwenye safari ya maisha, hasa inapokuja kwenye mafanikio, huwezi kukwepa kulipa gharama zinazohitajika.
Utalipa waziwazi na kupiga hatua kwenda mbele.
Au utaacha kulipa kwa sababu humudu na hapo kujizuia kupiga hatua.
Kwa vyovyote vile, lazima kuna gharama unalipa.

Huwa kuna kauli inasema wakati mwingine thamani ya kitu inapimwa kwa kukikosa.
Hivyo pia ndivyo inavyokuwa kwenye kulipa gharama.
Unalipa gharama kubwa zaidi pale unapokwama kulipa gharama ya kitu kwa sababu unaona huwezi kumudu.

Tukilinganisha gharama ya kufanya na ya kutokufanya, kwa hakika ya kutokufanya ni kubwa kuliko ya kufanya.
Kwa maneno mengine, huwezi kumudu kutokufanya kitu chochote ambacho kina mchango wa kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Lipa gharama mapema na kwa usahihi ili uweze kupiga hatua unazotaka kupiga.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe