💯KCM2324027; Zao.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Zao.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo uhuru ni zao la utulivu.
Huwezi kuwa huru kwenye maisha kama huna utulivu.
Kadiri unavyokuwa umevurugwa ndivyo pia unavyokosa uhuru.
Wale wenye nia ya kuwadhibiti na kuwatawala watu wengine, huwa wanahakikisha wanawaweka kwenye hali ya usumbufu.
Wanafanya kila kitu kuhakikisha watu hao hawapati utulivu kabisa.
Kwa sababu wanajua utulivu una nguvu kubwa ya kuwaweka watu huru.
Kama unataka uhuru mkubwa na kamili kwenye maisha yako, unapaswa kuanza kwa kujijengea utulivu mkubwa kwenye maisha yako.
Anza kwa kutokuruhusu jambo lolote lile kukupa taharuki.
Pokea kila kitu ukiwa na utulivu mkubwa na kuangalia nini unachoweza kufanya kwenye hali husika ili kupata matokeo mazuri.
Unapoteza uhuru wako wote pale unapotaharuki kwa jambo lolote lile.
Hiyo ni kwa sababu ukiwa na taharuki unakuwa hufikiri kwa usahihi na hivyo kuwa rahisi kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi na yanayogharimu.
Haijalishi nini kinaendelea kwenye maisha yako, kitu ambacho hupaswi kukubali kukipoteza ni utulivu wako.
Ukiweza kubaki na utulivu wako kwenye kila hali, unakuwa umefikia ukomavu ambao utakupa matokeo makubwa.
Kudumisha utulivu wako mara zote ni silaha muhimu sana unayoihitaji kwenye safari yako ya mafanikio.
Linda sana usipoteze silaha hii kwa namna yoyote ile.
Pale unapojikuta kwenye hali ya kuvurugwa au taharuki, jizuie usifanye maamuzi wala kuchukua hatua yoyote.
Badala yake fanya zoezi la kupumua kwa kina huku ukihesabu pumzi zako.
Fanya zoezi hilo mpaka pale utakapojisikia ukiwa na utulivu wa ndani.
Kila siku pata muda wa kukaa peke yako na kutahajudi pamoja na kutafakari kuhusu mambo yako mbalimbali.
Utashangaa jinsi ambavyo tayari unao uwezo wa kutatua mengi ukiwa na utulivu kuliko ukiwa umevurugwa.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu hofu zisizo sahihi. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/25/3251
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutenga muda tulivu kwa ajili yako ambao utakupa uhuru mkubwa.
Kocha.
💯