3254; Farasi wa kuchonga.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama umewahi kuwaona watoto wakiwa kwenye mchezo ambao wamepanda farasi wa kuchonga, wanakuwa na furaha sana.
Wanaona wakiwa wamepanda farasi anayekwenda mbio, lakini kiuhalisia hakuna mahali wanakuwa wameenda.
Mbio zinakuwa nyingi, lakini wanakuwa wamebaki pale pale.

Hivyo pia ndivyo watu wazima wengi wanavyoshindwa kwenye maisha.
Wanaonekana wakiwa ni wachapa kazi sana, lakini hakuna hatua ambazo wanakuwa wanapiga kwenye kile wanachofanya, iwe ni kazi au biashara.

Wanaweza kuwa wanawahi kufika maeneo yao ya kazi kila siku na kuchelewa kutoka.
Wakawa pia wanafanya kazi kwenye siku zote saba za wiki bila hata kupumzika.
Miaka inakwenda na hakuna hatua kubwa wanazopiga, wanakuwa wanazidi kurudi nyuma kadiri muda unavyokwenda mbele.

Mwisho wanashindwa kabisa, kama wapo kwenye biashara inakufa na kama wameajiriwa wanaikosa kazi.

Mtu akiwaangalia watu hawa kwa nje anashindwa kabisa kuelewa nini kimewatokea.
Kwa sababu wanaonekana kuwa ni wachapa kazi sana, waliojitoa hasa.
Lakini inakuwaje wameshindwa vibaya kiasi hicho?

Kitu ambacho kwa nje hakionekani ni kwamba watu hao wanakuwa wametingwa na kazi ambazo ni feki.
Kazi ambazo hazina mchango kwao kupiga hatua kubwa.
Zinaweza kuonekana ni kazi za kuwachosha, lakini haziwapi fursa ya kupiga hatua zaidi.

Na hiyo ndiyo dhana ya farasi wa kuchonga kwa watu wazima.
Wanajiona wametingwa kweli kweli, lakini hakuna mahali wanaenda.

Kwenye ajira ni mtu kuhangaika na majukumu ambayo ni ya kusukuma karatasi kwenda mbele.
Haya ni majukumu ambayo hayana matokeo makubwa na mapya kwenye taasisi ambayo mtu anafanya kazi.
Bali ni majukumu ya kawaida tu, ambayo yanafanya mtu asionekane ni mvivu, lakini hayaleti matokeo yoyote mapya na makubwa.

Kwenye hali ya kawaida, watu hao wataendelea kuwa na kazi, siyo kwa sababu wana mchango kwenye taasisi, bali kwa sababu kuwafukuza inakuwa gharama kwa taasisi kuliko kubaki nao.
Hivyo licha ya kuwa mzigo, bado unakuwa unaweza kuvumilika.

Ni kwenye nyakati ngumu ambapo taasisi haiwezi tena kubeba mizigo ndiyo watu wa aina hiyo wanapoteza kazi zao.
Pale taasisi inapokuwa na sababu za msingi za kupunguza watu, wanaoanza kuondolewa ni wale ambao wanaonekana kufanya sana kazi, lakini hawana mchango kwenye ukuaji wa taasisi.

Kwenye biashara, farasi wa kuchonga ni pale mtu anapohangaika na majukumu ambayo hayana mchango wa moja kwa moja kwenye kuingiza kipato.
Hapa mtu anatingwa na majukumu mengi yaliyopo kwenye biashara, lakini yanakuwa hayaleti kipato moja kwa moja.

Kwa nyakati ambazo ni nzuri kibiashara, bado biashara inaweza kubaki hai, kwa sababu wateja wanaokuwepo wanaendelea kununua.
Wananunua siyo kwa sababu ya maajabu yoyote, bali kwa sababu wameshazoea kununua.
Ni mpaka pale yanapotokea mabadiliko yanayowaathiri wateja na wakashindwa kununua kama walivyokuwa wamezoea ndipo biashara inaathirika sana.
Athari hizo ndizo zinazoua biashara nyingi.
Lakini kifo kinakuwa kilianza muda mrefu, kilichotokea ni kumalizia tu.

Njia ya kuondokana na farasi wa kuchonga ni kutumia kanuni ya 80/20.
Kwa kanuni hiyo unahakikisha unaweka kipaumbele kikubwa kwenye majukumu yenye tija kuliko majukumu ya kawaida.
Asilimia 80 ya juhudi zako unaweka kwenye majukumu yanayoleta matokeo makubwa kama ni kwenye kazi au kuleta kipato moja kwa moja kwenye biashara.

Unapokuwa na majukumu 10 ya kutekeleza, 8 yanapaswa kuwa yale yanayoleta matokeo makubwa na mawili yanayoleta matokeo ya kawaida.
Unapokuwa na masaa 10 ya kufanya kazi, masaa 8 yanapaswa kuwa ya majukumu makubwa na masaa mawili ya majukumu ya kawaida.

Kufanya kwa namna nyingine yoyote, tofauti na hapo ni kuchagua kupanda farasi wa kuchonga.
Ufajiona upo mbio sana, unafanya kazi sana, lakini unakuwa umebaki pale pale, hakuna mahali unakuwa unaenda.

Achana na kazi feki na fanya kazi halisi zenye mchango mkubwa.
Kwenye ajira fanya majukumu yanayoleta matokeo makubwa na ya tofauti.
Kwenye biashara fanya zaidi matokeo yanayoleta wateja wapya na kukuza zaidi mauzo.
Muda ni wako, nguvu ni zako na umakini ni wako.
Ni wewe utachagua kama utapeleka rasilimali hizo kwenye farasi wa kuchonga au farasi halisi.

Swali muhimu kwako kujiuliza, kutafakari na kushirikisha hapa ni hili; ni farasi gani feki ambao umewapanda kwa muda mrefu na kukwama eneo moja bila kukua?
Ni farasi gani halisia ambao umechagua kuwapanda sasa ambao watakupeleka kwenye matokeo makubwa zaidi?
Shirikisha majibu yako kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe