3256; Njia mbili.

Rafiki yangu mpendwa,
Maisha huwa yana njia kuu mbili ambapo lazima mtu uchague moja ambayo ndiyo utaisafiri kwa kipindi chote cha maisha yako.

Njia ya kwanza ni ya mtu kuwa na ndoto kubwa ambazo unazipambania mpaka kuzifikia.
Ndoto hizo zinakuwa ni kubwa sana kiasi cha kukutaka uweke kila ulichonacho katika kuzipambania.
Mtu anayechagua njia hii anakuwa hana budi bali kupuuza mengine yote ambayo hayana mchango kwake kufikia ndoto kubwa alizonazo.
Ni wachache sana wanaoichagua hii njia. Wengi hujaribu na kuishia njiani, kwa kushindwa kujitoa kwa namna inavyohitajika.

Njia ya pili ni njia ya usumbufu ambapo mtu anahangaika na kila kinachokuja mbele yake.
Wanaopita kwenye njia hii huwa wanaamini uwepo wa njia ya mkato ya kupata chochote ambacho mtu anataka bila ya kufanya kazi sana.
Hilo linawapelekea kila wakati kuwa na kitu kipya wanachokimbizana nacho, kwa kuamini hicho ndicho kimebeba mafanikio yao.

Kwa bahati mbaya sana, watu wengi huwa hawapati hata nafasi ya kuchagua ni njia ipi watakayotumia.
Badala yake huwa wanajikuta tayari wapo kwenye njia ya pili, njia ya kuhangaika na mambo mengi yasiyokuwa na tija kwa mtu.
Kwa sababu hivyo ndivyo walio wengi wanavyoendesha maisha yao, imezoeleka na hata kuonekana ndiyo njia bora na ya kipekee.

Watu wengi huwa hawajui kama njia ya kwanza ipo. Hivyo maisha yao yamekuwa yanaenda kwa mazoea ambayo ndiyo wale waliowazunguka wanaenda hivyo.
Wanaojua uwepo wa njia ya kwanza ni wale ambao tayari ndani yao wana msukumo wa kufanya mambo makubwa zaidi ya ilivyozoeleka. Hawa tayari huwa wanajikuta kwenye njia ya kwanza na wakipambania kile wanachokitaka sana.

Wapo pia ambao huwa wanajua uwepo wa njia ya kwanza kupitia kujifunza.
Lakini pamoja na kujifunza na kujua, uhalisia huwa ni tofauti kabisa na mipango ambayo mtu anakuwa ameiweka.
Hivyo wengi wa wanaojifunza njia ya kwanza huwa hawaendi nayo kwa muda mrefu mpaka kupata matokeo makubwa. Wanapoanza kuifanyia kazi njia hiyo wanategemea matokeo ya haraka. Ni pale wanapokutana na changamoto au matokeo kuchelewa ndiyo safari huwa inaishia hapo na wanahamia kwenye njia ya pili.

Rafiki, kama bado hujaichagua njia ya kwanza kama njia yako kuu, fanya hivyo sasa.
Chagua kitu kimoja ambacho ndiyo utakipambania kwa maisha yako yote.
Kisha kipe kitu hicho kipaumbele namba moja kwenye maisha yako.
Vitu vingine vyote vinafuata baada ta kitu hicho, hivyo hata ufanyaji wa vitu vingine, haupewi nafasi ya kuvuruka kilicho kikuu.

Kubali maisha yako yazamie kwenye kile kikubwa kimoja unachotaka kufikia.
Kuwa bora sana kwenye kitu hicho kiasi cha kuweza kupuuza mengine yote.
Toa thamani kubwa sana kwa wengine kupitia kile ulichochagua kufanya, kiasi cha watu hao kuwa tegemezi kwako kwenye kukamilisha mambo yao.

Kuyatoa maisha yao kwa ujumla ili kuweza kufikia ndoto kubwa unazokuwa nazo ni njia yenye uhuru mkubwa kwa anayeielewa njia hii na kukubaliana nayo.
Kataa kufuata mkumbo wa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija, kwa sababu hilo ndiyo linalowapoteza walio wengi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe