3260; Siyo matokeo, bali muda.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anapambana kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Na njia ambazo watu wanatumia kujenga mafanikio nayo zinatofautiana.

Njia nyingi tofauti za mafanikio zinaweza kuwafikisha watu kwenye mafanikio wanayoyataka. Lakini hilo linategemea zaidi mkazo ambao watu hao wanao, kama ni kwenye matokeo au muda.

Wanaoweka mkazo kwenye matokeo ni wale ambao wapo tayari kufanya chochote kile ili tu kupata matokeo wanayokuwa wanayataka. Kwa msukumo huo, wengi huwa tayari hata kufanya vitu ambavyo ni kinyume na sheria.
Watu wa aina hii, hata wakipata matokeo waliyokuwa wanayataka, huwa hayadumu kwa muda mrefu. Mara nyingi njia wanazokuwa wametumia kupata matokeo hayo zinawapoteza zaidi.

Wanaoweka mkazo kwenye muda ni wale wanaoangalia matokeo wanayoyapata yanaweza kudumu kwa muda mrefu kiasi gani. Wanahakikisha wanatumia njia ambazo zinawapa matokeo yanayodumu kwa muda mrefu zaidi. Hili linawafanya watumie njia ambazo ni sahihi tu na hilo kupelekea wachelewe kuyapata matokeo.

Njia rahisi ya kupima mkazo wa mtu uko wapi, angalia ni kwa haraka kiasi gani anataka kupata matokeo.
Kama mtu anataka kupata matokeo ya haraka bila kuweka juhudi kubwa, jua huyo mkazo wake upo kwenye matokeo.
Lakini kama mtu anataka kupata matokeo yanayodumu bila kujali itamchukua muda kiasi gani kuyapata, huyu mkazo wake upo kwenye muda.

Kitu kikubwa sana kuhusu safari ya mafanikio ambacho wengi huwa hawakipi uzito ni kutokuwepo kwa njia ta mkato.
Tangu enzi na enzi watu wamekuwa wanatafuta na kutumia njia za mkato ili kupata kile wanachotaka.
Lakini mara zote matokeo yamekuwa yanakuja tofauti, kwa watu kupoteza zaidi kuliko wanavyonufaika.

Kwa ngazi ambayo wewe umeshafikia, hili la kutokuwepo kwa njia ya mkato kwenye mafanikio unapaswa kuwa unalielewa na usikubali kulaghaiwa kwa namna ya tofauti.
Usihangaike na njia za mkato, bali kaa kwenye njia kuu na ya uhakika, ambayo itakupa matokeo hata kama ni kwa kuchelewa.

Tukiangalia kwa mfano wa fedha, unaweza kucheza kamari na ukashinda kwa kupata fedha nyingi. Lakini je una uhakika kiasi gani wa kurudia kucheza tena na kupata ushindi wa aina hiyo? Jibu ni hakuna uhakika wowote, kwa sababu huna udhibiti wa juhudi unazoweka wala matokeo unayopata.

Usiangalie tu matokeo unayoyapata, bali pia angalia yanaweza kudumu kwa muda kiasi gani. Unachopaswa kuzingatia ni kuzalisha matokeo ambayo yanakuwa ni ya uhakika na yanayodumu kwa muda mrefu zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe