💯KCM2324037; Jipende.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Jipende.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaona jinsi ambavyo kujipenda wewe mwenyewe kwanza kulivyo ufunguo wa mengine makubwa kwenye maisha.

Mapenzi ndiyo yanaendesha dunia.
Watu huwa wanafanya kitu chochote kile kwa sababu kuu mbili;
Moja ni wanapenda kufanya kitu hicho.
Na mbili ni kufanya kitu hicho kunawapa kile wanachopenda.
Ni vigumu sana kwetu binadamu kuchukua hatua kama hakuna mapenzi yanayohusika.

Pamoja na kuendeshwa na mapenzi kwenye yale tunayofanya, bado huwa tunakutana na magumu na changamoto ambazo mapenzi tunayokuwa nayo kwenye kile tunachofanya au matokeo tunayopata hayawezi kuvuka.

Hapo ndipo unapokuwa unahitaji mapenzi ya juu zaidi ambayo ni kujipenda wewe mwenyewe kwanza.
Unapoanza kwa kujipenda wewe mwenyewe, mengine yote yanakaa mahali pake.
Hakuna magumu au changamoto zozote zinazokuwa na nguvu ya kukukwamisha kwenye chochote unachofanya.

Kama unataka kufanya makubwa kwenye maisha yako, ni lazima uanze kwa kujipenda sana wewe mwenyewe.
Lazima ujipende wewe kuliko kitu kingine chochote.
Ni kupitia kujipenda sana ndiyo unaweza kujiamini na kujikubali.
Na kupitia kujiamini na kujikubali unaweza kukabiliana na chochote kwenye maisha yako.

Imani kuu inayopaswa kuyaendesha maisha yako inapaswa kuwa ya upendo. Hapo unaanza kwa kujipenda wewe mwenyewe kwanza, kisha unawapenda wale wanaokuzunguka na mwisho unapenda kile unachofanya.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyapangilia mapenzi yako vizuri ili uweze kupata chochote unachotaka.

Ukianza kwa kujipenda wewe mwenyewe, hakuna kinachoweza kukuangusha au kukukatisha tamaa.
Ukiwapenda wengine, inakuwa rahisi wao kukupa kile unachotaka.
Ukipenda kile unachofanya, utakifanya kwa muda mrefu zaidi hata kama matokeo hayaji kama ulivyotarajia.

Kujipenda na kujikubali ni moja ya njia za kuachilia breki ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa.
Zingatia haya mara zote ili kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujikumbusha ushindi ambao tayari umeshaupata. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/05/3261

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujipenda sana wewe mwenyewe na kusukumwa na upendo huo kufanya makubwa zaidi.

Kocha.
💯