3262; Utabiri mzuri wa tabia za watu.

Rafiki yangu mpendwa,
Tabia za watu ni kama ngozi, wakishakuwa nazo huwa ni vigumu sana kubadilika.
Tabia ikishajengeka huwa inakuwa ni sehemu ya maisha ya mtu.
Hata kama mtu anatamani sana kubadilika, kwa upande wa tabia ni lazima awe amedhamiria kweli na kujitoa kuteseka.

Kwa sababu hiyo basi, badala ya kuwauliza watu watafanya nini, angalia wameshafanya nini.
Ukiwauliza watakujibu kwa maneno mazuri, ambayo ndiyo wanatamani wangekuwa hivyo.
Kumjua mtu vizuri angalia ni vitu gani amefanya huko nyuma.
Kwani utabiri mzuri wa tabia za watu zijazo ni tabia zilizopita.

Kama unataka watu watakaokupa ushindi, anza na ambao tayari walishapata ushindi huko nyuma.
Ni rahisi zaidi kwao kupata ushindi mwingine kuliko yule anayetamani kupata ushindi lakini hajawahi kupata.

Chochote kile unachotaka kukipata kutoka kwa watu, epuka sana kuwauliza au kuamini yale wanayokuambia.
Badala yake angalia tabia zao za nyuma kwenye hilo eneo.
Kama watu wamewahi kufanya kitu huko nyuma, ni rahisi kwao kufanya tena.
Lakini kama hajawahi kufanya, itakuwa ni vigumu kwake kufanya, hata kama ameahidi makubwa kiasi gani.

Watu huwa ni waongeaji wazuri,
Huwa wanaahidi mengi sana.
Lakini inapofika kwenye utekelezaji, ndiyo huja na sababu na visingizio vingi.
Tunajua dhahiri kwamba mtu anaweza kutoa matokeo au akatoa sababu, siyo vyote kwa pamoja.
Watoaji wa matokeo watakupa matokeo, haijalishi nini kitatokea.
Na watoaji wa sababu watatoa sababu bila ya kujali nini kimetokea.

Kosa kubwa sana ambalo huwa tunalifanya kwa watu ni kutamani wawe vile tunavyotaka wawe.
Hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea kwa namna ambavyo mtu anataka.

Watu huwa wanaendelea kuwa vile walivyo. Hivyo kama hutaki kukwama na kukwazika, anza na watu ambao tayari wana tabia unazotaka badala ya kuanza na ambao unataka wabadilike.

Zingatia hili kwa watu wote unaojihusisha nao, kuanzia wafanyakazi, wateja, wenza n.k. Anza na wale ambao tayari wameshaonyesha tabia unayoitaka badala na kuanza na wanaokupa ahadi, hata kama ni ahadi nzuri kiasi gani.
Hilo litakusaidia uwaepuke wale ambao siyo sahihi kwako.

Usiishie tu kwenye maneno,
Nenda hatua ya ziada kujua matendo yao ya nyuma.
Maana hayo ndiyo kiashiria kizuri cha matendo yajayo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe