KCM2324039; Machale.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#AlhamisiYaUbunifu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Neno la leo; Machale.
Leo ikiwa ni #AlhamisiYaUbunifu tunaona jinsi ambavyo machale yanavyokuwa sehemu ya ubunifu.
Kuna wakati huwa unapata msukumo wa kufanya kitu fulani, lakini unakuwa huna sababu za msingi za kwa nini unataka kukifanya.
Watu wanapokutaka uyaelezee maamuzi yako unashindwa kufanya hivyo.
Lakini ndani yako unajua ndiyo kitu sahihi kufanya. Na unapokifanya, unapata matokeo mazuri.
Msukumo huo wa ndani wa kufanya kitu ambao hatuwezi kuuelezea ndiyo tunaita machale.
Hayo huwa yanatokana na uzoefu mkubwa ambao mtu anakuwa amejijengea kwenye eneo husika.
Kutokana na uzoefu huo, kuna mambo yakienda tofauti unaona kwa haraka na kupata msukumo huo wa tofauti.
Ni kwa njia hii ndiyo machale yamekuwa sehemu ya ubunifu. Mara nyingi sana pale unapopata msukumo wa ndani wa kufanya kitu, huwa ni ubunifu unajaribu kukuonyesha nini unapaswa kufanya.
Kwenye hali kama hizo, unapaswa kuyasikiliza machale yako na kuchukua hatua.
Ubunifu huwa ni kitu cha kipekee sana.
Ubunifu hauwezi kufundishwa wala kulazimishwa.
Ni pale watu wanapokuwa na utulivu na kujisikiliza wao wenyewe ndiyo wanaweza kufungua ubunifu mkubwa ulio ndani yako.
Usipuuze machale unayoyapata bali yazingatie, kuna uzoefu ulio ndani yako ambao huwezi kuuelezea. Uzoefu huo ndiyo unakuwezesha kuona vitu vya tofauti na jinsi ya kuvitumia ili kuzalisha matokeo bora kabisa.
Jisikilize sana wewe mwenyewe, una mengi ya kujua na kuzingatia ili uweze kupiga hatua kubwa.
Na kama tunavyojua, kila mtu ni mbunifu, ila wengi wamekuwa hawatumii ubunifu ulio ndani yao kwa sababu huwa hawajisikilizi. Na hata wakijisikiliza huwa hawajiheshimu kiasi cha kutekeleza yale wanayopata msukumo wa kufanya.
Achilia breki za kukosa ubunifu ambazo zimekuwa zinakukwamisha kwa mara zote kuzingatia machale unayokuwa nayo. Kuna kitu unakuwa umeona ambacho huwezi kukielezea. Hicho ndicho kilichobeba ubunifu na fursa ya kufanya makubwa.
Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu sababu za kuacha. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/07/3263
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kusikiliza machale yako na kuyatumia kuwa na ubunifu zaidi.
Kocha.