3264; Gharama ya makosa.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inayosema usimkatishe adui yako akiwa anafanya makosa. Hiyo ni kwa sababu makosa yake yanakuwa na manufaa kwako.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa upande wako, makosa unayofanya unaishia kuwanufaisha zaidi wengine.

Kwa kila kosa unalofanya, jua kuna wengine ambao wananufaika kupitia makosa yako.

Lengo lako halipaswi kuwa kutokufanya makosa kabisa, bali kuepuka makosa ya kizembe na kuepuka kurudia makosa yale yale kila mara.

Makosa ya kizembe ni yale ambayo mtu hajali kwenye kile anachofanya hivyo anaacha kutumia njia sahihi ambazo zingepunguza makosa, badala yake anafanya kilicho rahisi kwake na kuishia kufanya makosa makubwa.

Kurudia makosa ni pale mtu anapofanya kitu kile kile na kwa namna ile ile. Huu ndiyo unaitwa ujinga na watu huishia kulipa gharama kubwa.
Utachukuliaje pale unapotozwa mara mbili au zaidi kwenye kitu chochote kile?
Kwa hakika utaumia, sasa kwa nini urudie makosa yale yale na kulipa gharama zile zile.

Kukosea ni mara moja, tena pale unapokuwa umeweka tahadhari zote. Gharama unazoingia kwenye kosa la kwanza ni ada unayokuwa umelipa kwenye mafunzo unayokuwa umepata.
Kama utarudia tena kosa hilo hilo, unakuwa umepoteza ada hiyo bure.

Kwa kuwa kila makosa unayofanya yana gharama, chukua tahadhari pale unapofanya kitu kwa mara ya kwanza. Na ukishafanya kosa, jifunze kwa kina kuhusu kosa hilo kiasi kwamba kamwe hutaweza kulirudia tena.

Nenda hivyo na utaweza kuwa mtu mwenyewe hekima na kufanya makubwa kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe