đź’ŻKCM2324042; Pozi.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

đź’Ż Neno la leo; Pozi.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii inapaswa kuwa kitufe cha kupozi au kusimamisha kwa muda heka heka za maisha.
Kitu chochote kinachokwenda kwa kasi kubwa, huwa kinahitaji kupumzishwa kwa muda ili kuweza kwenda kwa muda mrefu bila kuchoka na kushindwa.
Hivyo pia ndivyo maisha yalivyo, yanakwenda kwa kasi sana kwa majukumu mengi tuliyonayo kila siku, huku muda wa kuyatekeleza ukiwa hautoshi.
Kwa kasi hiyo kubwa ya maisha, kama tutaenda nayo bila kujipa mapumziko, tutachoka haraka na kuishia njiani.
Ndiyo maana ni muhimu kila baada ya siku sita, tunapaswa kupumzika kabisa kwa siku moja.
Lengo ni kukusanya nguvu kubwa zaidi za kuendelea na kasi tunayoenda nayo.
Kwa hesabu za kawaida unaweza kuona siku moja ya mapumziko kwenye siku 7 ni kubwa sana na ya upotevu mkubwa.
Lakini hilo ni kama utaangalia kwa kipindi kifupi. Ukiangalia kwa kipindi kirefu, utaona dhahiri kwamba njia pekee ya kudumu kwenye hiyo kasi ni kuwa na mapumziko ya kila mara.
Kwa siku sita, kama utahitajika hata kukesha, kesha, lakini tenga siku moja ya kupumzika, siku ambayo hutaenda kwa kasi unayoenda nayo kila siku.
Na siku nzuri ya kufanya hivyo ni kwenye siku ambayo wengi pia wana mapumziko, ambayo kwa wengi ni jumapili.
Jumapili ni siku ambayo wengi hawana matarajio ya kukuta wengi kwenye shughuli zao. Hivyo unaweza kuwa huru kuitumia vile unavyotaka bila ya kuharibu matarajio ya wengine.
Nenda kasi uwezavyo, lakini usisahau kuweka pozi kila baada ya muda ili usije ukamaliza kabisa mafuta na safari yako kufika ukingoni kabla hata ya kufika ulikopanga kufika.
đź’ŻHatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kukosa imani kwenye kile unachofanya. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/10/3266
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kuweka pozi kwenye heka heka zako ili kukusanya nguvu za kuendelea kwa kasi kubwa zaidi.
Kocha.
đź’Ż
Asante Sana Kocha Dr Makirita Amani.
Hakika ni Muhimu Sana kuweka pozi.
Zamani nilikuwa nikiamini kufanya kazi siku Saba za wiki ni jambo jema lakini kumbe haipo hivyo.
Tangu nimeanza kuweka “pozi” siku ya jumapili nimejikuta nikiianza jumatatu Kwa Shauku kubwa Sana na hii pia imeniongezea ufanisi katika kazi.
Jumapili kwangu ikuwa kama siku ya kuuchaji mwili wangu kuwa tayari Kwa wiki nzima inayofuata.
Asante.
LikeLiked by 1 person
Hakika,
Kama ambavyo simu zinahitaji kuchajiwa, ndivyo pia na miili yetu inahitaji chaji.
Siku ya jumapili ni maalumu kwa hilo.
LikeLike