3270; Ushauri na nyakati.

Rafiki yangu mpendwa,
Ushauri ambao watu wanapewa kwenye safari ya mafanikio ambayo wapo, huwa unategemea sana ni wakati au hatua gani mtu huyo yupo.

Ushauri unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa mtu kama ndiyo anaanza. Lakini ushauri huo huo usiwe na manufaa kama mtu ameshaanza kupata ukuaji mkubwa.

Wakati unaanza, ambapo unakuwa chini kabisa, ushauri wa jumla utakuwa na manufaa makubwa kwako. Kwani unakupa mwanga wa nini unapaswa kufanya na kipi kinakuwa kipaumbele kwako.

Wakati unakua zaidi, ambapo unakuwa umeshapiga hatua fulani, unahitaji ushauri maalumu. Kwenye hatua hiyo ushauri wa jumla hauwezi kukusaidia tena. Kama utaendelea kutumia ushauri wa jumla kwenye wakati wa ukuaji, utapunguza kasi ya ukuaji unaokuwa nao.

Unapokuwa unaanza, unahitaji tu kuchukua hatua. Hizo ndiyo zinakuwa na nguvu ya kumweka mtu kwenye uelekeo sahihi wa kufanikiwa.

Unapoendelea kukua, unahitaji kuchukua hatua ambazo ni maalumu kulingana na pale mtu alipo ukilinganisha na anakoenda.

Tuchukue mfano wa ushauri wa kufanya kazi kwa juhudi.
Kama mtu ndiyo anaanza, ushauri wa fanya kazi kwa juhudi kubwa una manufaa kwake.
Kwa sababu mwanzoni mtu anafanya mambo mengi na yote yana mchango, kila juhudi anayoongeza inaleta matokeo mazuri.

Lakini mtu huyo huyo anapokuwa ameanza kukua, ushauri wa fanya kazi kwa juhudi hauwi na manufaa kwake. Anaweza kuweka juhudi kubwa ya kazi na asikue kwa sababu anakuwa ameweka juhudi hizo kwenye eneo lisilo sahihi.

Hivyo kwenye hatua kama hiyo, mtu anahitaji ushauri maalumu, unaoendana na hali yake na matokeo anayotaka. Mfano wa ushauri maalumu wa mtu kupewa ni fanya kazi kwa juhudi kubwa kujenga timu itakayoleta mafanikio makubwa.

Kwa kuelekeza juhudi sehemu sahihi, inaleta matokeo makubwa kuliko kuzitawanya kama awali.

Kwenye maisha, mara zote anza na hatua za msingi na za jumla, kisha endelea kuboresha kadiri unavyokwenda.
Epuka sana kwenda kwa mazoea, kufanya leo kile ulichofanya jana.
Kwenye kila hatua jifanyie tathmini ni ushauri upi wa jumla umekufikisha hapo, kisha angalia ni ushauri gani maalumu unaohitaji ili kukua zaidi ya hapo.

Kwa kila ushauri unaoupata kutoka kwa wengine, usikimbilie tu kuufanyia kazi, hata kama ushauri huo umekuwa na manufaa kwao.
Unapaswa kujitathmini kwanza hatua uliyopo sasa na kule unakotaka kufika. Kisha jiulize kama ushauri unaopewa ni wa jumla au maalumu kwako.

Kuna wakati mtu unaweza kufanyia kazi ushauri unaopata na ukazidi kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.
Hiyo inatokana na kutumia ushauri wa jumla wakati ulihitaji ushauri maalumu.

Jua ushauri unaohitajika kwenye kila nyakati za safari ili uweze kuwa na ukuaji endelevu mara zote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe