💯KCM2324049; Hasira.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Hasira.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii inapaswa kuwa ya kukupa hasira ya kujisukuma zaidi kwenye siku nyingine za wiki.
Safari ya mafanikio huwa inashangaza sana.
Unakuta mtu anaanzia chini kabisa, anapambana sana kufanikiwa, ili astaafu mapema.
Kwa juhudi kubwa anazoweka, anafanikiwa sana.
Anaamua kustaafu kwa sababu maisha yake yanaweza kwenda vizuri hata kama hafanyi kazi moja kwa moja.
Siku za mwanzo kwenye kustaafu zinakuwa ni siku za furaha kwa sababu mtu anafanya chochote anachotaka.
Lakini huwa haiwachukui watu muda mrefu kabla hawajagundua kustaafu ni makosa makubwa kwao.
Wanajikuta maisha yao yakikosa maana kama hawafanyi kazi moja kwa moja.
Na hilo huwa linawafanya wengi kurudi kwenye kufanya kazi japo hawalazimiki kufanya hivyo.
Ni mpaka pale watu wanapouonja uhuru wa kutokufanya kazi ndiyo wanagundua kazi ni sehemu muhimu ya maisha ya mtu.
Sasa wewe huhitaji kusubiri mpaka ustaafu ndiyo ugundue umuhimu wa wewe kuendelea kufanya kazi hata kama umeshafanikiwa.
Unachotakiwa kufanya ni kutumia siku ya jumapili kama siku ya kustaafu.
Iishi kila jumapili kama vile umestaafu kabisa na hufanyi tena shughuli unazofanya.
Zoezi hilo litakufanya uone umuhimu wa wewe kuendelea kufanya shughuli zako hata kama hulazimiki kufanya hivyo.
Lakini pia unaweza kuitumia siku ya jumapili kutengeneza hasira ambayo itakusukuma kwa wiki nzima.
Unachohitaji kufanya ni kuitumia jumapili kinyume kabisa na unavyotumia wiki yako nzima.
Jumapili fanya yale ambayo utasukumwa kutumia wiki nzima kuyalipa.
Kwa mfano kama huwa unajali sana muda, siku ya jumapili poteza muda mwingi kwenye mambo yasiyo na tija, ili upate hasira ya kurekebisha hilo kwa wiki nzima inayofuata.
Iishi siku ya jumapili kwa namna ambayo utaona umeipoteza, ili unapoianza wiki nyingine uwe na hasira ya kurekebisha yote uliyofanya jumapili na kupelekea kupoteza.
Hasira huwa ina msukumo mkubwa kwetu.
Na pale tunapoona tumepoteza, huwa tunafanya zaidi kufidia.
Tahadhari ni usifanye mambo ambayo yana madhara ya kudumu kwako na kwa wengine. Maana hayo hayataweza kurekebishwa na msukumo unaotokana na hasira unayokuwa umeipata.
Kuziishi siku zote za wiki kwa usawa kunapelekea kuwa na maisha ya mazoea na ya kurudia yale yale kila siku.
Lakini kuifanya jumapili kuwa siku ya tofauti na ambayo unaipoteza, kunakusukuma kutumia siku za wiki kufidia, kitu ambacho kinakusukuma zaidi.
Itumie kila jumapili yako kupata hasira ya kuzitumia vizuri zaidi siku nyingine za wiki.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kutokuyafanya mambo kuwa magumu zaidi ya yalivyo sasa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/17/3273
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kujenga hasira itakayokusukuma kuishi kwa utofauti kwenye siku za wiki zinazofuata.
Kocha.
💯