3274; Hatari ya mafanikio.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunapambana sana kufanikiwa, lakini hakuna kitu ambacho ni hatari kwenye maisha kama mafanikio.

Hatari ya mafanikio inaanzia ndani ya mtu na kutoka nje yake pia.
Hatari ya nje kwenye mafanikio ni kushambuliwa na wengine, ambao kwa sehemu kubwa wanakuwa wanakuonea wivu.

Hatari ya ndani ya mafanikio ni kujisahau na kulewa sifa kitu ambacho kinapelekea kuharibu kile ulichojenga.

Kwenye moja ya mahojiano yake, Charlie Munger amewahi kusema hakuna kitu kinachoshindwa haraka kama mafanikio. Alieleza kwamba watu wengi wanapofanikiwa huwa wanaanza kuhangaika na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao, kitu kinachopelekea wapate anguko kubwa.
Alimalizia akisema kilichowafanya wao na mbia mwenzake Warren Buffet kufanikiwa ni kuwa tayari kukaa na kutokufanya chochote pale ambapo hakukuwa na kitu sahihi kwao kufanya.

Kuna funzo kubwa sana ka kuondoka nalo hapo.
Iko hivi, watu wengi wanapokuwa wanaanzia chini kabisa, huwa wanakuwa na nidhamu kubwa na inayowasukuma kufanya makubwa na kufanikiwa.
Lakini wakishafanikiwa, wanaacha nidhamu hiyo na kukaribisha anguko.

Wengi wakati wanafanikiwa wanapambania kitu kimoja kwa ukubwa sana mpaka wanapata matokeo makubwa.
Wakishapata matokeo makubwa kwenye kitu hicho kimoja, wanapata dharau na kudhani wanaweza kila kitu.
Hilo linawapelekea kujiingiza kwenye mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao na yanawapelekea kupata anguko kubwa.

Rafiki, chochote kilichokufikisha kwenye mafanikio, unahitaji kukifanya mara mbili ili uweze kubaki kwenye mafanikio hayo.
Unaya wa mafanikio ni ukilegeza tu kidogo, anguko ni kubwa na la haraka.

Tunaona wengi wanaopambana na kupata mafanikio makubwa wakiwa wanayapoteza yote. Hiyo ni kwa sababu walidhani wakishafanikiwa ndiyo wanaweza kupumzika vile wanavyotaka. Kumbe kiuhalisia, ukishafanikiwa unahitajika kufanya kazi mara mbili ya ulivyokuwa unafanya kabla hujafanikiwa.
Kwa sababu hapo unakuwa na kazi mbili, ya kwanza ni kulinda mafanikio ambayo tayari unayo usiyapoteze, kazi ambayo ni ngumu. Na kazi ya pili ni kuendelea kuyakuza mafanikio hayo kwa sababu kubaki pale ulipo ni kudumaa na kurudi nyuma.

Watu wengi hupambana sana kuyajenga mafanikio. Lakini wanakuwa hawajui kuna kazi kubwa zaidi ya kuyalinda hayo mafanikio baada ya kuwa wameyapata.

Hakuna wakati unaohitaji kuwa na tahadhari kubwa kama pale unapokuwa umepata mafanikio makubwa.
Kwani ni vigumu sana kujua kipi ni kweli na kipi siyo kweli.
Ukishafanikiwa, kila mtu anakuwa anayawinda mafanikio yako.
Hivyo usipokuwa na tahadhari, ni rahisi sana kupoteza kila kitu.

Nakuacha na kauli mbili za Kiswahili ambazo mara zote zitakukumbusha hatari ya mafanikio ili usijisahau na kuanguka.

Moja; ‘Kadiri nyani anavyopanda juu zaidi, ndivyo matako yake yanavyoonekana wazi.’
Ufafanuzi; unapofanikiwa, makosa yako yanaonekana wazi zaidi na kwa wengi kuliko ukiwa hujafanikiwa. Jua hilo na uweze kwenda nalo vizuri.

Mbili; ‘Kadiri unavyokwenda juu zaidi ndivyo anguko linavyokuwa na kishindo kikubwa.’
Ufafanuzi; unapokuwa na mafanikio makubwa ni rahisi kuanguka na unapoanguka, madhara yanakuwa makubwa kuliko ukiwa huna mafanikio makubwa.

Rafiki yangu mpendwa, mafanikio ni mazuri, lakini kama hutaujua ukweli huu uliojifunza hapa, mafanikio yatakuwa machungu sana kwako.
Zingatia haya ili uweze kujenga mafanikio utakayodumu nayo kwa muda mrefu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe