3277; Hakuna tatizo.

Rafiki yangu mpendwa,
Matatizo, changamoto na vikwazo huwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Pamoja na vitu hivyo kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, watu wamekuwa wanashindwa kuvifanyia kazi na matokeo yake ni kukua zaidi.
Hilo ndiyo limekuwa linasababisha maisha kuwa magumu zaidi.

Njia rahisi ya kutatua tatizo lolote kwenye maisha yako ni kuamua kwamba huna tatizo hilo.
Hapa unachofanya ni kulibadili tatizo na kuliona kwa namna tofauti.
Badala ya kuliangalia kama tatizo, unaliangalia kama hatua ya kuchukua au kitu cha kupuuza.
Hii haimaanishi kwamba unayakimbia matatizo, bali unayakabili kwa namna ya tofauti.

Watu wengi huwa wanayakabili matatizo kama matatizo, kitu ambacho kinayakuza na kuyafanya kuwa magumu zaidi.
Kwa kuliona tatizo kama tatizo inalifanya kuwa kubwa na kuonekana ni gumu zaidi kwako kulitatua.

Kwa njia ya kutatua tatizo kwa kulichukulia siyo tatizo, unalifanya kuwa dogo kuliko lilivyokuwa linaonekana. Unafanya hivyo kwa njia mbili.

Njia ya kwanza ni kuangalia ni hatua ipi unayopaswa kuchukua kwenye tatizo husika.
Kama ipo njia ya kuchukua, unaacha kuliangalia kama tatizo na unaangalia ile hatua inayopaswa kuchukuliwa.
Kwa mfano kama una tatizo ambalo linaweza kutatuliwa na kiasi fulani cha fedha, unaacha kuliangalia kama tatizo na kuangalia kama hitaji la kiasi hicho cha fedha. Hapo wajibu wako unabadilika na kuwa kupata kiasi hicho cha fedha kinachohitajika.

Njia ya pili ni kama hakuna hatua unayoweza kuchukua ili kutatua tatizo husika, yaani tatizo hilo halitatuliki, unalipuuza kabisa. Unalichukulia kama sehemu ya maisha badala ya kuliona kama tatizo. Hapo unapunguza ukali wake na kukupa nguvu ya kuendelea na mambo mengine unayoweza kuyafanya.
Kuhangaika na tatizo ambalo huwezi kulitatua ni matumizi mabaya ya rasilimali zako. Likubali tatizo kwamba siyo tatizo ili maisha mengine yaweze kuendelea.

Kwa kila tatizo unalokutana nalo kwenye maisha yako, tumia njia hizo mbili kulifanya kutokuwa tatizo na utaweza kuchukua hatua sahihi zinazokuwezesha kwenda mbele zaidi.

Kama una tatizo na unaweza kulitatua, huna tatizo, bali una hatua unayopaswa kuichukua ili kuvuka hapo ulipo.
Na kama una tatizo na huwezi kulitatua, huna tatizo, bali una hali unayopaswa kuikubali na kuipuuza.
Yachakate matatizo yako kwa njia hizo mbili ili uweze kumalizana nayo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe