💯KCM2324055; Kichocheo.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumamosiYaUtulivu

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI kitakusaidia kuondokana na usumbufu wa simu. Kipate kwa mawasiliano 0678 977 007



💯 Neno la leo; Kichocheo.

Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo utulivu ni kichocheo cha uvumbuzi.

Akili zetu zina uwezo mkubwa sana wa kuvumbua vitu mbalimbali.
Kila uvumbuzi tunaouona leo, ulifanywa na watu kama sisi.
Tena wengi wao wakiwa hawana akili kubwa sana.

Wote walioweza kufanya uvumbuzi mkubwa, walikuwa na utulivu mkubwa ndani yao.
Walizipa akili zao muda wa kukaa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu zaidi.
Kwa kukaa kwenye kitu kwa muda mrefu, kuna vitu vya tofauti walivyoona, ambavyo walivichanganya pamoja na kuweza kuja na uvumbuzi wa tofauti.

Huwa kuna hadithi kwamba mwanasayansi Isaac Newton aligundua nguvu ya mvutano ya dunia akiwa amekaa chini ya mti na kuona tunda linaanguka chini. Alijiuliza kwa nini tunda hilo halikwenda juu na hapo ndipo ukawa mwanzo wa kugundua nguvu ya mvutano ya dunia.

Pamoja na kwamba Newton alikuwa na akili, kama isingekuwa utulivu, asingeweza kuunganisha kuanguka kwa tunda na nguvu ya mvutano ya dunia.

Kukosa utulivu imekuwa breki inayowazuia wengi kufanikiwa kwa kuwafanya wasiweze kuja na uvumbuzi wa tofauti.
Na kwenye zama tunazoishi sasa, hali ni mbaya zaidi kwa sababu ni vigumu sana mtu kupata muda wa kuwa tulivu.
Hata kama mtu yuko peke yake, bado anakuwa ameambatana na usumbufu wa simu yake janja ya mkononi.

Kwa muda wote kuzungukwa na usumbufu, akili inahangaika na mambo yasiyokuwa na tija na hivyo kushindwa kuja na uvumbuzi wa tofauti.

Kuondokana na hilo na kuweza kuchochea uvumbuzi wa vitu vipya, tunapaswa kutenga muda wa sisi kuwa tulivu.
Tunapaswa kutenga muda ambao tutakaa kwa utulivu bila ya kusumbuliwa na chochote.
Tunaweza kuona ni muda tunaoupoteza, lakini ni muda wenye manufaa makubwa sana kwetu.

Achilia breki ya kukosa utulivu ili uweze kuja na uvumbuzi utakaokuwezesha kufanya makubwa.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu mafanikio na kupendwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/23/3279

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutenga muda wa kuwa na utulivu ili kuchochea uvumbuzi mpya.

Kocha.
💯