3290; Unachoshindana nacho.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanalalamikia ushindani kuwa mkali na kuwa kikwazo kwao kufanikiwa kwenye biashara.
Wanaona kama isingekuwa ushindani basi wangekuwa wamepiga hatua kubwa sana.

Lakini huo siyo ukweli.
Kama kuna ushindani pekee ambao unawakwamisha watu kwenye biashara basi ni uvivu na uzembe.
Uvivu na uzembe ndiyo vikwazo vikubwa kwa biashara nyingi kufanikiwa.

Uvivu ni kujua kinachopaswa kufanywa, lakini kutokukifanya.
Na uzembe ni kufanya kitu kwa makosa, huku mtu akiwa anajua kabisa jinsi ya kufanya kwa usahihi.

Biashara yoyote ile inaweza kupata mafanikio makubwa sana kama itafanya vitu viwili kwa ukubwa na msimamo; kuwa na wateja wengi na kuwafuatilia wateja hao kwa uhakika.

Hakuna ushindani wowote unaoweza kuizuia biashara kuwafikia wateja wengi.
Wala ushindani hauwezi kuzuia biashara isiwe na ufuatiliaji wa karibu na uhakika wa wateja.

Kwa sababu ya uvivu na uzembe, biashara nyingi hazifanyi hayo mawili kwa weledi mkubwa. Lakini pia watu hawapendi kujiona wao ni wavivu na wazembe, ndiyo maana lawana zitapelekwa kwa wengine wengi ila siyo kwa mtu mwenyewe.

Chukua mfano ni mara ngapi kwenye biashara wateja wamekuambia wakiwa tayari watakutafuta. Je ni mara ngapi wateja hao wamekutafuta kweli?
Hata kwa upande wa pili, ukiwa kama mteja, ni mara ngapi umekuwa unawaambia wauzaji utawatafuta ukiwa tayari. Lakini mpaka sasa bado hujamtafuta.

Unajionea hapo jinsi uvivu na uzembe vilivyo na athari kubwa kwenye mafanikio ya mtu.
Wewe acha kutumia sababu za nje kwenye hayo.
Badala yake angalia ndani yako ni kwa namna gani umekuwa unajikwamisha wewe mwenyewe.
Jinasue kwenye mkwamo huo kwa kuwa tayari kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachokifanya ili kupata matokeo makubwa.

Usiwe mvivu wala mzembe,
Chapa kazi sana, utavuka mengi unayoyaona ni kikwazo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe