3291; Kupambania unachotaka.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa hawapati kile wanachotaka, siyo kwa sababu hawawezi kupata, bali kwa sababu wanashindwa kukipambania kweli.

Kila kitu ambacho mtu anakitaka, kinawezekana kabisa kupatikana.
Lakini hakiwezi kupatikana kirahisi.
Lazima mapambano makali sana yaweze kuvukwa na yule anayetaka.

Ni mapambano makali kwa sababu kuna vikwazo vingi vya kuvuka.
Kwanza ni vikwazo binafsi, ndani ya mtu kunakuwa na uvivu na uzembe unaomfanya ashindwe kuweka juhudi za kutosha.
Kuvuka uvivu na uzembe wa ndani lazima mtu apambane sana.

Mbili ni vikwazo vya wengine.
Wale wanaokuzunguka wanataka uendelee kuwa ulivyo ili wasikupoteze na kushindwa kukutumia.
Hivyo watakuwa na upinzani mkali sana kwako ili kukuzuia usiendelee na mapambano ya kupiga hatua kubwa zaidi.

Tatu ni vikwazo vya dunia.
Unapoiambia dunia unayataka makubwa, kwanza inakucheka kwa jinsi tu ulivyodhani unaweza kupata hayo makubwa.
Halafu inaanza kukuletea kila aina ya vikwazo ili kupima kama kweli unaweza kuyahimili mambo makubwa unayoyataka.

Vikwazo vyote unavyopitia ni muhimu sana katika kukuandaa kupokea unachotaka na kuweza kudumu nacho.
Kwa sababu ni kile unachokipambania hasa kwenye maisha yako ndiyo unakithamini na kuweza kudumu nacho kwa muda mrefu.

Chochote unachokipata kwa urahisi bila kupambana hasa, huwa hukithamini, hata kama ni kikubwa kiasi gani.
Hivyo unaishia kukipoteza kwa haraka sana.

Hivyo unapokutana na magumu kwenye kupata kile unachotaka, usikate tamaa.
Badala yake furahia kwa sababu unakwenda kuwa imara zaidi na kuweza kupata ambacho utadumu nacho kwa muda mrefu.

Ukikitaka kitu kweli, usijali ni magumu kiasi gani unakutana nayo, wala usiangalie ni muda kiasi gani inakuchukua kukipata.
Wewe jua utakipata, halafu kinachofuata ni kukipambania kwa uhakika zaidi.
Unapopambana ukiwa huna namna nyingine zaidi ya kupata ushindi, utapata ushindi ambao ni mkubwa sana.

Pambania unachotaka, ndiyo njia pekee ya kukipata kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe