💯KCM2324068; Kujidanganya.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#IjumaaYaMawasiliano

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Kujidanganya.

Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaona jinsi ambavyo tatizo kubwa sana kwenye mawasiliano ni kujidanganya kwamba yamekamilika.

Mawasiliano yamekuwa na changamoto kubwa kwa sababu ya kujidanganya kwa pande zote mbili ambazo zinashiriki mawasiliano hayo.
Upande unaowasilisha unadhani kwamba umeeleweka, wakati siyo.
Na pia upande unaopokea unadhani kwamba umeelewa, kumbe siyo.

Mawasiliano mengi huwa yanamalizika kwa pande zote mbili zikiwa mbali kuliko zinavyodhani.
Lakini pande zote zinadhani mawasiliano yamekamilika.
Ni kwenye utekelezaji ndiyo ombwe la kutokuelewana vizuri linaonekana.

Njia ya kuvuka changamoto hii ni kuacha kujidanganya na kudhani mawasiliano yamekamilika.
Badala yake ni kuhakikisha kweli mawasiliano yamekamilika na pande zote zimeelewana.

Upande unaowasilisha unapaswa kuhakikisha umeeleweka.
Siyo kwa kudhania, bali kwa kuuliza upande uliopokea mawasiliano umeelewaje.
Pale mtu anapotoa mrejesho wa jinsi alivyoelewa ndiyo unaweza kuona kama kweli ameelewa au la.

Upande unaopokea mawasiliano unapaswa kuhakikisha umeelewa vizuri.
Siyo kwa kudhania, bali kwa kutoa mrejesho kwa upande uliotoa mawasiliano.
Upande unaopokea mawasiliano unapaswa kueleza jinsi ulivyoelewa ili kuhakikisha kama ndivyo upande uliowasilisha ulikuwa unakusudia.

Kama tunavyoona hapa, kukamilika kwa mawasiliano ni jukumu la pande zote mbili.
Hivyo ushirikiano wakati wa mawasiliano ni muhimu sana ili kuelewana.
Kwenye mawasiliano usijidanganye kwa kudhani yamekamilika, bali kila upande unapaswa kwenda hatua ya ziada kuhakikisha kweli mawasiliano yamekamilika.

Mawasiliano kutokukamilika ni moja ya breki zinazowazuia wengi kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Wewe achilia breki hiyo kwa kuhakikisha kila mawasiliano unayohusika yamekamilika kwa usahihi, iwe ndiye unayewasilisha au kupokea.
Siyo tabia ya wengi kujipa wajibu kwenye kukamilika kwa mawasiliano, ila fanya hivyo, kwa sababu hilo lina matokeo makubwa na mazuri.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuvutiwa na maneno. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/05/3292

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuacha kujidanganya mawasiliano yamekamilika kwa kuhakikisha badala ya kudhania.

Kocha.
💯