Kitu kimoja ninachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kwamba maisha yangu yamejengwa kupitia usomaji wa vitabu. Kila kitu ambacho nimekifanya kwenye maisha yangu, sehemu kubwa ya mwongozo nimepata kutoka kwenye vitabu mbalimbali ambavyo nimesoma.
Mimi ni muumini mkubwa sana wa usomaji wa vitabu na ninatamani sana kila mtu aliye hai asome sana vitabu. Hiyo ni kwa sababu matatizo na changamoto nyingi ambazo watu wanapitia, tayari zina majibu yake kwenye vitabu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa siyo wapenzi wa kusoma vitabu. Na kwa zama hizi za simu janja na mitandao ya kijamii, hali ndiyo inazidi kuwa mbaya, kwani watu wanashindwa kabisa kusoma vitabu.
Kwa kuwa maisha yangu yamejengwa kupitia usomaji wa vitabu, hapa nakwenda kushirikisha uzoefu wangu binafsi kwenye hili ili uweze kukusaidia na wewe kujenga tabia hii kama bado hujawa nayo.

Nimekuwa napenda kusoma vitabu tangu nikiwa mtoto. Nakumbuka hata nilipokuwa shule ya msingi, nilikuwa nikisoma kila kitabu cha hadithi nilichokuwa nakutana nacho shuleni. Nikiwa darasa la nne nilijipa changamoto ya kusoma Biblia yote mpaka niimalize, na nilienda kitabu kwa kitabu ila sikuweza kuimaliza kwa mfululizo niliokuwa nimeweka.
Nikiwa sekondari, niliendelea kuwa nasoma vitabu vinavyopatikana shuleni. Nakumbuka kwenye somo la Kiingereza, upande wa Literature, Mwalimu alifundisha vitabu viwili tu kwa ajili ya kujibia mtihani wa taifa (Mine Boy na Is It Possible). Lakini kwa kuwa shuleni kulikuwa na vitabu zaidi, mimi nilisoma vitatu vya ziada (Things Fall Apart, The River Between na Three Suitors One Husband). Kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha nne, swali lililohusu kitabu lilikuwa tofauti kwa hiyo waliokuwa wamesoma vitabu vichache walikuwa na uwanja mdogo. Ila mimi kwa kuwa nilisoma vitabu vingi, nilikuwa na uwanja mpana na nikaweza kujibu vizuri. Kwenye matokeo nilipata alama A ya somo la Kiingereza, japo nilikuwa mkondo wa sayansi.
Niliporudi mtaani baada ya kusimamishwa Chuo kikuu mwaka 2011, niliona nafasi ya kurudi chuoni ni ndogo. Hivyo nikajiuliza; nawezaje kufanikiwa kwenye maisha hata kama sina ‘degree’? Swali hilo ndiyo lilifungua ulimwengu mpya wa vitabu vya maendeleo binafsi kwangu. Mwaka 2012 nilianza kusoma vitabu, na vitatu ambavyo nilianza navyo na vikanifungua sana ni RICH DAD POOR DAD, THINK AND GROW RICH na THE RICHEST MAN IN BABYLON.
Kwa jinsi vitabu hivyo vilivyonibadili, nakumbuka mwaka huo 2012 niliandika kwenye mitandao ya kijamii niliyokuwa natumia kwamba natoa bure vitabu hivyo kwa nakala tete kwenye email. Watu zaidi ya 100 walinitumia email zao, kitu ambacho sikutegemea kabisa. Na hapo ndipo safari ya uandishi na kufundisha eneo la maendeleo binafsi ilipoanza rasmi, baada ya kuona kuna uhitaji wa maarifa ya maendeleo binafsi.
Tangu mwaka 2012 nimekuwa nasoma na kusikiliza vitabu, angalau viwili kila wiki. Kuna wakati naenda zaidi ya hapo, hasa ninapokuwa natafiti kuandika kitabu. Lakini huwa sikubali wiki iishe sijasoma kitabu hata kimoja. Mpaka sasa nimesoma vitabu zaidi ya elfu moja, maarifa ya msingi yamekuwa yanajirudia rudia kwenye vitabu hivyo vingi, ila kwa namna ya tofauti na inayoleta uelewa zaidi.
Nimekuwa naendesha programu mbalimbali za kuhamasisha usomaji wa vitabu kwa watu. Watu wamekuwa wanaanza programu hizo kwa shauku kubwa, ila inapofika wakati wa kusoma vitabu na kushirikisha, wengi wamekuwa wanapotea. Mwaka 2014 nilianzisha programu ya Tanzania Voracious Readers, lengo likiwa ni kujenga kiu kubwa ya usomaji kwa watu. 2018 nilianzisha TANO ZA MAJUMA YA MWAKA na baadaye SOMA VITABU TANZANIA. Pia kuna programu ya TUSOME PAMOJA DAILY na nyingine. Kwa kila programu ambazo naendesha, usomaji umekuwa ni kiungo muhimu ambacho nimekuwa nahakikisha kinakuwepo ili watu waweze kujijenga na kuwa bora zaidi.
Katika vitabu hivyo vingi sana ambavyo nimesoma mpaka sasa, kuna ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa wa moja kwa moja kwenye kuyabadili kabisa maisha yangu. Kwenye mfululizo wa vipindi vya ONGEA NA KOCHA, kila wiki nitakuwa nashirikisha kitabu kimoja kilichobadili maisha yangu na mambo unayoweza kuondoka nayo ya kwenda kufanyia kazi ili maisha yako yawe bora pia.
Kama na wewe ungependa kuyabadili maisha yako kupitia usomaji wa vitabu, zingatia mambo haya ya msingi kutokana na uzoefu wangu.
1. Penda kusoma vitabu kutoka ndani yako. Usisome kuiga wengine au kuwaambia wengine umesoma. Soma kwa mapenzi na utanufaika sana.
2. Kuhusu ni vitabu gani usome, anza na vile unavyopenda kusoma kwanza, bila ya kujali vina mchango kwako au la. Naval Ravikant anasema; soma vitabu unavyopenda mpaka utakapopenda kusoma vitabu. Hivyo kama riwaya za ujasusi ndiyo unapenda kusoma, soma hizo mpaka usomaji utakapokuwa tabia kwako ndiyo uende kwenye vitabu vingine.
3. Kuhusu kupata muda wa kusoma vitabu, muda haujawahi kupatikana, bali muda unatengwa. Kila siku tenga muda usiopungua nusu saa kwa ajili ya kusoma kitabu. Unaweza kupanga muda wowote kwenye siku yako, ila itapendeza kama utaufanya muda wa kusoma kuwa asubuhi na mapema kabla fujo za dunia hazijaanza.
4. Ukisoma andika yale unayojifunza na hatua unazoweza kuchukua kwenye hayo unayojifunza. Unaelewa zaidi pale unaposoma na kuandika kuliko ukisoma tu bila kuandika.
5. Chukua hatua mara moja kwenye yale unayojifunza kupitia usomaji wa vitabu. Ukuaji wa huduma zote ninazofanya ni kwa sababu huwa nachukua hatua mara moja pale ninapojifunza kitu ninachoona kina mchango. Hilo limekuwa linafanya kila wakati niwe nakuja na vitu vipya ambavyo vimefanya huduma kukua zaidi.
6. Kuhusu gharama za vitabu, tenga bajeti ya maendeleo binafsi ili kila mwezi uweze kununua vitabu. Na kama huwezi kabisa kumudu vitabu, soma vitabu vya bure vinavyopatikana mitandaoni. Na kama yote yatashindikana, basi soma vitabu vya dini, kama Biblia na Kurani, vina mafunzo mengi sana na unaweza kuvipata hata bure kabisa, kama kweli unataka kusoma.
7. Usisome ili kumaliza vitabu vingi, bali soma ili kuelewa na kuwa bora. Kila unapomaliza kusoma kitabu, jiulize wewe baada ya kusoma kitabu unatofautianaje na wewe kabla ya kusoma kitabu hicho. Ni muhimu sana uhakikishe unajiona ukibadilika kupitia usomaji wa vitabu.
8. Kuhusu kusoma nakala ngumu (hardcopy) au tete (softcopy), chagua kile kinachokufaa wewe. Usijifunge sana kwenye upande upi, muhimu ni uweze kujifunza. Muhimu sana ni uwe na kitabu kila mahali unapokuwepo. Hivyo unaweza kuwa na nakala nguvu vichache na nakala tete vingi pale unapokuwa kwenye mizunguko yako ili unapohitaji kusoma usikwame.
9. Usiazime watu vitabu, hasa vya nakala ngumu, huwa hawaendi kuvisoma na mbaya zaidi hawakurudishii. Kama mtu amependa kitabu ambacho amekuona nacho, mwelekeze uliponunua na yeye akanunue. Kama hawezi kununua, basi hakihitaji kweli. Na hata ukimwonea huruma ukampa, hataenda kukisoma. Hili nimejifunza kwa maumivu sana, kama utabisha na kufanya, jiandae kuumia.
10. Kuwa na vitabu vilivyosomwa (Audio Books) na sikiliza pale unapokuwa kwenye maeneo ambayo usomaji ni mgumu. Uzuri simu za sasa zina uwezo wa kubeba mamia ya vitabu vilivyosomwa. Pia kuna spika za masikioni ambazo ni ndogo na hazina hata nyaya. Hivyo unaweza kuvaa spika zako za masikioni na kusikiliza vitabu ukiwa kwenye foleni au unasubiri kitu. Mimi binafsi popote ninapokuwepo lazima niwe na spika za masikioni, kwa ajili ya kusikiliza vitabu pale fursa inapopatikana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA kuhusu kubadili maisha yako kupitia usomaji wa vitabu nimeeleza haya kwa kina zaidi. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na uchukue hatua ya kuwa mpenzi wa vitabu ili uweze kuyaboresha maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
http://www.amkamtanzania.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.