3294; Onekana, weka kazi na sikiliza.

Rafiki yangu mpendwa,

Kwa kipindi ambacho nimekuwa natoa hii huduma ya mafunzo na ukocha, nimejifunza mengi sana kuhusu watu.
Nimejifunza hayo kwa nadharia na kwa vitendo pia kutoka kwenye tabia halisi za watu.

Kwenye nadharia nimekuwa najifunza mara kwa mara vitu vitatu vinavyohitajika ili huduma ya ukocha iweze kuwa na manufaa kwa mtu.
Na hapo kuna mambo matatu ambayo lazima yawepo.

Moja ni lazima mtu aonekane, hapa ni sawa na kusema ahudhurie mafunzo na kufuata taratibu zote zilizopo.
Kama mtu haonekani au mahudhurio yake siyo mazuri, hawezi kunufaika.

Mbili ni lazima mtu aweke kazi sana, hapa mtu anapaswa kutekeleza yale anayojifunza ili kupata matokeo. Kwa sababu matokeo hayawezi kuja kimiujiza, lazima kazi kubwa iwekwe.

Tatu ni kusikiliza, hapa mtu anapaswa kuweka ujuaji pembeni na kusikiliza kile anachoelekezwa na kukifanyia kazi. Bila usikivu mtu hawezi kunufaika na huduma ya ukocha.

Kwenye uhalisia, nimekuwa naona jinsi watu wanavyoenenda na mambo hayo matatu na kudumu kwenye huduma na mara zote imekuwa ikileta matokeo ya uhakika.

Wengi wanapoanza huduma wanakuwa wanatekeleza mambo yote matatu, hata kama hawajaambiwa.
Wanaonekana mara zote kwa kushiriki mambo yote yanayohusu mafunzo.
Wanaweka kazi kubwa kwa kufanyia kazi yote wanayojifunza.
Na wanakuwa na usikivu, wakielekezwa cha kufanya wanakifanya.
Hayo matatu yanawawezesha watu kupiga hatua kubwa sana kuliko ambavyo wamewahi kupiga kwenye maisha yao.

Na baada ya mtu kupiga hatua na kupata mafanikio kiasi, ndipo mambo huanza kubadilika.
Kwa ambao wanaendelea na mambo hayo matatu bila kuacha, wanadumu kwenye huduma na kuendelea kupiga hatua kubwa sana.
Mafanikio yanaendelea kuwa makubwa kwao na huduma inazidi kuwa ya thamani.
Lakini hawa ni wachache sana.

Wengi wakishapata mafanikio kiasi, wanaanza kulega kwenye mambo hayo matatu ya msingi.
Wanaanza kutokuonekana, hawahudhurii mafunzo kama awali. Wanaweza kuwa na visingizio mbalimbali, lakini mafanikio wanayokuwa wamepata ni kama yanawatinga na wanaona mafunzo siyo muhimu tena kwao.

Wanapunguza kuweka kazi kwa kuona wameshavuka hatua ya kujituma sana. Kwa mafanikio wanayokuwa wamepata na kuwa na watu wanaowasaidia kwenye mambo mengi, wanajiona wameshavuka ngazi ya wao kuhangaika kuweka kazi. Hilo linapunguza kasi yao ya mafanikio.

Halafu sasa, wanaacha kusikiliza. Wanakuwa na ujuaji mwingi. Baada ya kupiga hatua fulani, wanaona mafunzo ni ya chini kwao kwa hatua ambazo wamepiga. Wengine kwa kuona wameshafanikiwa kifedha kuliko Kocha, wanaona hana tena cha kuwaambia.

Mara zote, wale ambao hawazingatii mambo makuu matatu, huwa hawadumu kwenye huduma kwa muda mrefu.
Wengi hupotea. Na kwenye upotevu huo kuna ambao huweza kuendeleza mafanikio waliyoyapata. Lakini wengi huyapoteza mafanikio hayo.
Na pale wanapoanguka na kurudi tena, hawawi kama walivyokuwa awali.

Nimekuwa naona hili kwa muda mrefu na nimekuwa najidanganya mwenyewe kwa kuwapa watu muda nikidhani wataweza kubadilika.
Lakini hali imekuwa inaenda hivyo. Wanaozingatia yote matatu wanadumu na wasiozingatia hata moja tu wanapotea.

Baada ya kupingana na asili kwa muda mrefu bila ya mafanikio, nimeamua kukubaliana nayo.
Hivyo basi, nitafanya kazi na mtu pale tu atakapotekeleza mambo hayo matatu; KUONEKANA, KUWEKA KAZI na KUSIKILIZA.

Pale mtu anapoacha hata kimoja tu, hapo hapo naacha mara moja kufanya naye kazi.
Sitapoteza muda zaidi kusubiri mtu abadilike.
Ni anazingatia mambo yote matatu na kuwepo au anayaacha na kuondoka.

Hili halina ugumu wowote, ni unaonekana kwa kuhudhuria mafunzo yote, unaweka kazi kwa kutekeleza unauojifunza na kusikiliza kwa kuacha ujuaji.
Anayetaka hasa anafanya bila kuchoka.
Asiyetaka hatafanya, hata iweje.

Je wewe upo tayari kuzingatia hayo matatu, mara zote bila kuacha?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe