Kila binadamu anao uwezo mkubwa sana ndani yake. Lakini kwa bahati mbaya sana, wengi wamekuwa wanatumia sehemu ndogo sana ya uwezo huo.

Sababu kubwa ya wengi kushindwa kutumia uwezo wao ni kutokujua kama upo. Yaani mtu anakuwa na uwezo mkubwa ndani yake, lakini hajui hata kama upo.

Na hilo linajidhihirisha kwenye mambo mengi, ambayo watu wanafanya kwa kawaida, lakini pale wanapokuwa kwenye hali inayowataka wafanye zaidi, wanafanya.

Maisha ya zama hizi ni rahisi sana ukilinganisha na miaka mingi iliyopita. Watu wengi wanaishi kwenye usalama mkubwa tofauti na maisha ya watu kwenye karne nyingi zilizopita.

Miaka mingi iliyopita, binadamu waliishi kwenye nyakati ngumu. Hivyo miili yao ilijengwa kuweza kukabiliana na ugumu wa nyakati hizo. Fikiria enzi watu wanaishi maeneo yenye wanyama wakali na walioweza kuwadhuru muda wowote.

Kwenye zama hizi, hatari hizo nyingi zimeondolewa kabisa, lakini bado ule uwezo wa kukabiliana na magumu upo ndani yetu. Swali ni je watu wanatumiaje uwezo huo?

Majibu ni ya kusikitisha, watu wanatumia uwezo kujikwamisha badala ya kupiga hatua. Mfano mzuri ni hofu. Wakati ambapo binadamu walikuwa wanaishi kwenye nyakati ngumu, hofu ilihitajika ili kuwawezesha kujiokoa na hatari mbalimbali. Lakini kwenye zama hizi ambapo hatari zimepungua, watu wanatumia hofu kwenye mambo ambayo hayana hatari kubwa kwenye maisha yao.

Kwa mfano mtu anayehofia kuongea mbele ya watu au anayehofia kukataliwa, anatumia nguvu kubwa ya mwili kwenye hofu hizo, ambazo hata hazina hatari yoyote kwenye maisha yake.

Hivyo basi, ili mtu kuweze kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yake, zoezi la kufanya Tahajudi au kama linavyojulikana kama Meditation ni muhimu sana. Hili ni zoezi linalompa mtu utulivu mkubwa na kuweza kujisikiliza yeye mwenyewe, kitu kinachomsaidia kujitambua na kuweza kufanya makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza msingi mkuu wa tahajudi na jinsi inavyokuwezesha kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako. Hiki ni kitu ambacho kila mtu anapaswa kukifanya kila siku ili kuendelea kuwa karibu yake mwenyewe na kufanya makubwa.

Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na uanze kufanya tahajudi ili kutumia uwezo wako mkubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.