3297; Uko sahihi kabisa.

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye hii safari ya kujifunza, kufundisha na kukochi watu kwenye eneo la mafanikio, naendelea kujifunza mengi sana.

Moja ya hivyo ninavyojifunza ni mtazamo hasi ambao watu wengi wanao kwenye kupata mafanikio.

Imekuwa ni imani yangu na nguzo kuu ya mafundisho yangu kwamba kila mtu anaweza kujenga mafanikio makubwa bila ya kujali anaanzia wapi.
Yaani hata kama mtu anaanzia chini kabisa, anaweza kujenga mafanikio makubwa sana kwenye maisha yake kama ataamua na kujitoa kweli.

Kipindi cha nyuma, nilipokuwa nawaambia watu wanaweza kufanya makubwa na wakabisha kwamba hawawezi, nilikuwa nawabishia kwamba wanaweza.
Na hapo walizidi kunipa sababu za mafanikio kutokuwezekana kwao.
Hapo tulichoshana sana na mwisho kila mtu alibaki na msimamo wake.

Ni mpaka pale nilipojifunza kwamba kila mtu yupo sahihi kadiri ya fikra zake ndiyo niliacha kusumbuka na hilo.
Nilijifunza hilo kupitia kauli ya Henry Ford aliyesema kama unafikiri unaweza au unafikiri huwezi, upo sahihi.

Baada ya kujifunza hilo nikajiambia nitakuwa nawakubalia watu kwenye kile wanachofikiri.
Na hapo jambo la kushangaza sana lilitokea. Watu pia walikataa pale nilipowakubalia.

Kwa mfano nilipomwambia mtu anaweza kujenga mafanikio makubwa na akasema hilo haliwezekani, badala ya kumbishia nakubaliana naye.
Namwambia uko sahihi, kwa hali yako, huwezi kabisa kupata mafanikio makubwa.
Na hapo tena anaanza kubisha. Anabisha kwamba siyo kweli hawezi kupata mafanikio. Anaeleza kama akipambana ataweza kufanikiwa.
Na hapo nakubaliana naye tena, kwamba yupo sahihi, apambane na atafanikiwa.

Nimejifunza kwa njia hiyo ya kukubaliana na watu hatuchoshani na mwisho wa siku kila mtu anapata kile anachotaka na kudhamiria kweli.
Kwa kukubaliana na mtu inamweka kwenye upande wa kutaka kudhihirisha kile kilicho ndani yake hasa.
Wakati kubishana naye, atataka tu kupata ushindi kwa kusimamia chochote anachoweza.

Badala ya kuwabishia na kuwapa ushindi huku mimi nikishindwa, nawakubalia na kila mtu anapata ushindi.

Kwa hiyo rafiki yangu, kwa lolote lile, uko sahihi.
Kama unakubali upo sahihi na kama hukubali pia upo sahihi.
Ni wewe tu unaamua nini hasa unachotaka na dunia inakupa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe