3301; Kupata na kukosa.

Rafiki yangu mpendwa,

Kuna watu huwa wanadhani maisha yanaendeshwa kwa bahati.
Kwamba wenye bahati wanapata wanachotaka na wasiokuwa na bahati wanakosa.

Lakini ukweli ni kwamba maisha yanaendeshwa na kupata au kukosa.
Ni labda unapata kile unachotaka au unakikosa.

Ili upate unachotaka, lazima kuna juhudi unazopaswa kuweka.
Ni pale watu wanapokuwa hawaoni juhudi za mtu kwa nje ndiyo wanadhani ana bahati.
Kwa kuwa wanaona mtu amepata kitu kirahisi, wakati wao wamekikosa, ndiyo wanadhani kwamba ana bahati.

Wakati mwingine kurudia rudia kitu mara nyingi bila kuchoka kunamfanya mtu kupata, baada ya kuwa amekosa mara kadhaa.
Hilo pia huwa linachukuliwa na wengi kama bahati, lakini ni vile wanakuwa hawajaona jinsi ambavyo mtu amerudia rudia kwa muda mrefu bila kuchoka.

Kiuhalisia ni kwamba inapokuja kwenye matokeo ambayo watu wanayapata, hakuna bahati.
Kwani hata michezo inayoitwa ya kubahatisha, bado pia nyuma yake siyo bahati, ni kupata na kukosa.

Mchezo wowote wa kubahatisha, huwa una matokeo ya aina moja ambauo ni sahihi na yanayotabiriwa na watu wengi.
Anayepatia matokeo hayo ndiyo anakuwa mshindi. Hivyo nyuma ya huo mchezo ni kupata na kukosa.
Ni labda umepata matokeo yaliyo sahihi au umeyakosa, hakuna bahati.

Njia ya kuelezea dhana ya bahati kwa namna rahisi ya kueleweka na wengi ni maandalizi kukutana na fursa.
Mtu anaonekana kuwa na bahari pale maandalizi aliyokuwa nayo yanapokutana na fursa.
Na hapo unaendelea kuona bado msingi ni kupata na kukosa.
Kwamba matokeo hayaji tu kimiujiza, kuna namna yanakuwa yamesababishwa.

Hivyo basi, kama unataka kuwa na bahati kwenye maisha yako, kuwa mtu wa kufanya. Mara zote fanya, ukipata matokeo sahihi endelea kufanya na ukikosa matokeo sahihi boresha na fanya tena.
Ndivyo matokeo makubwa yanavyojengwa kwenye maisha, kwa kufanya bila kuacha.

Kwa kuwa kuna watu ambao hawawezi kukaa bila kufanya kitu fulani, hao wamekuwa wanapata matokeo mazuri kuliko wengine.
Kwa nje wamekuwa wanaonekana kama ni wenye bahati.
Lakini kwa ndani ni watu wa kufanya bila kuacha na hivyo kuwa kwenye nafasi ya kupata zaidi kuliko wengine.

Mara zote fanya,
Utapata na kuona una bahati,
Au utakosa na kuendelea kufanya,
Bila kuchoka wala kukata tamaa,
Na kadiri unavyofanya,
Ndivyo unavyokuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata.
Chochote unachotaka kupata, usisubiri kije kwa bahati, bali kifanyie kazi na utakipata kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe