3302; Kujidanganya kwenye fedha.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna watu ambao huwa wanajidanganya kwenye fedha kama wale ambao hawana fedha nyingi.
Huwa wanajidanganya kama sehemu ya kujifariji.
Lakini kujidanganya huko bado huwa hakuondoi ukweli kwamba hawana fedha na fedha ni muhimu.

Fedha ni muhimu sana kwenye maisha, kwa sababu inanunua vitu vingi tunavyohitaji kwenye maisha yetu.
Lakini cha thamani zaidi ambacho fedha inaweza kununua ni uhuru kamili wa mtu.
Uhuru kamili wa mtu ni pale anapoweza kuchagua nini afanye, wakati gani na kushirikiana na watu gani.

Haupo huru kama bado unalazimika kufanya shughuli zinazokuingizia kipato cha kuendesha maisha moja kwa moja.
Kwa kuwa tu na utegemezi wa kipato hicho cha moja kwa moja, kunakufanya usiwe huru. Kwani utajikuta unalazimika kufanya vitu usivyokuwa tayari kufanya au kushirikiana na watu ambao hufurahii kufanya nao kazi.

Kuishi kipato kwa kipato, yaani kutegemea kipato cha moja kwa moja kwenye kuendesha maisha ni utumwa mkubwa sana.
Kwani unalazimika kufuata matakwa ya chanzo hicho cha fedha unazotegemea kuendesha maisha yako. Chanzo hicho kikikatika mara moja, unajikuta kwenye wakati mgumu sana.

Kuwa na madeni ni utumwa mwingine mkubwa sana wa kujitakia. Kwa sababu unakuwa umetumia kipato ambacho hukuwa nacho, lakini unakilipa kwa gharama kubwa zaidi.
Kila deni huwa lina riba, hivyo unalipa zaidi ya ulivyotumia.
Ukishakuwa na madeni maana yake unawafanyia wengine kazi. Hata ukazane kiasi gani, bado unabaki na kiasi kidogo cha fedha.

Kupata uhuru kamili wa maisha yako ni ondokana na madeni yanayokugusa wewe moja kwa moja, yaani yale yanayoathiri kipato chako.
Halafu kuwa na uwekezaji ambao unakuingizia faida inayotosheleza kuendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.

Moja ya vitu vitakavyokusaidia sana kwenye fedha ni kuwa mkweli kwako binafsi juu ya utegemezi kwenye kipato na madeni unayokuwa nayo.
Kama upo kwenye madeni, kwanza acha kuendelea kuyatengeneza na weka mpango wa kuyalipa yote.
Na kama huna uwekezaji, anza mara moja na kuujenga uwekezaji wenye manufaa kwako.

Huwezi kufikia uhuru wa kifedha na utajiri kwa kujidanganya wewe mwenyewe.
Matokeo yanaonyesha dhahiri kama unachofanya ni sahihi au la.
Tumia matokeo unayopata kuboresha hatua unazochukua ili kupata matokeo ya tofauti na yenye tija.

Anza kuwa mkweli kwako mweyewe kuhusu hali yako ya kifedha.
Kuwa mkweli ni wapi unapoanzia na nini unapaswa kufanya ili kufikia uhuru unaoutaka.
Ukiacha kujidanganya na ukawa mkweli kwako, utaweza kujinasua popote unapokuwa umekwama.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe