💯KCM2324079; Kutokujali.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Kutokujali.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaona jinsi ambavyo hupaswi kupoteza nguvu zako kubadili maoni ya watu juu yake, badala yake kufanya unachofanya na kutokujali wengine wanakuchukuliaje.

Kila mtu ana maoni yake ya jinsi gani unapaswa kuwa, nini unapaswa kufanya na unapaswa kufanyaje.
Lakini maoni yote hayo ni ya nje na ya kubahatisha, hayahusiani kabisa na kile unachokitaka hasa kutoka ndani yako.

Unaweza kujaribu kuyabadili maoni hayo ya wengine, kwa kuwaambia nini hasa unaweza na unataka kukamilisha kwenye maisha yako. Lakini bado watu hawatakusikiliza, wataendelea kutaka uwe vile wanavyotaka wao.

Kama utakuwa hujikubali wewe mwenyewe kwa vile ulivyo na yale unayotaka, itakuwa rahisi sana kwako kutetereka na kufuata hayo maoni ya wengine.
Na ukishaacha njia yako na kufuata maoni ya wengine, safari yako inakuwa imefika tamati.

Unachopaswa ni kuhangaika na kile tu unachotaka wewe na kutokujali kabisa kuhusu maoni ya wengine.
Unawaacha wengine waendelee kujifurahisha kwa hayo maoni waliyonayo kuhusu wewe, lakini wewe unaendelea kupambana na yako.

Kwa sababu mara nyingi sana, watu wenye maoni makali kwako, wao wenyewe hawajui hata ni nini wanachotaka kwenye maisha yao.
Je unataka kweli usumbuliwe na kukwamishwa na watu wa aina hiyo?
Unataka kweli uache kufanya makubwa unayoyaona kwenye fikra zako na uwafuate ambao hawajui hata ni nini wao wenyewe wanataka?

Hebu jikubali sana wewe mwenyewe, jua upo sahihi kwenye kile unachotaka hata kama maoni ya wengine ni tofauti.
Usijali sana kuhusu maoni ya wengine, jali zaidi wewe kufika kule unakotaka kufika.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu wa kumfuata mwenzake. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/16/3303

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuacha kuhangaika kubadili maoni ya wengine, badala yake kufanya yako na kutokujali wengine wanakuchukuliaje.

Kocha.
💯