3304; Kukwepa kuwajibika.

Rafiki yangu mpendwa,
Unakumbuka ulipokuwa mdogo na ukatamani sana kuwaonyesha watu jinsi unavyoweza kufanya mambo yanayofanywa na watu wazima.
Na baada ya kufanya hivyo yakageuka kuwa sehemu ya majukumu yako.
Yaani baada ya kuonyesha kwamba unaweza, ukaanza kupangiwa uyatekeleze.

Ni hali hiyo ya kuwajibika ndiyo imekuwa inapelekea watu wengi kutokuwa tayari kuonyesha uwezo mkubwa ulio ndani yao.
Unakuta mtu anaweza kabisa kufanya mambo makubwa, lakini anaficha hilo kwa sababu anajua akishaonyesha kwamba anaweza kufanya, atategemewa aendelee kufanya makubwa mara zote.
Sasa kwa kuwa watu wengi hawapendi kuwajibika, wanaona ni bora wafiche ule uwezo wao ili wasitegemewe kwa makubwa.

Pamoja na hilo kuwa changamoto, kwa wengi wenye uwezo kuuficha ili wasiwajibike nao, pia ni fursa nzuri kwa ambao wapo tayari kuwajibika.
Kwa kuchagua kuonyesha wazi uwezo mkubwa ulio ndani yako na watu wengi kuwa tayari kukutegemea kwenye uwezo huo unapata mafasi kubwa ya kutegemewa na walio wengi.
Ni kupitia kutegemewa huko ndiyo unaweza kufanya mambo makubwa na ya tofauti na kuzalisha matokeo bora na ya kipekee.

Kila unapokutana na watu wanaoficha uwezo wao mkubwa ili wasiwajibishwe nao, wewe ona fursa ya kuonyesha ulichonacho ili kuweza kufanya makubwa.

Kuwa kihere here wa kuonyesha wengine yote unayoweza kufanya, ili sifa zako zisambae kwa wengi zaidi.
Sifa zako zinapowafikia wengi, unakuwa na umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutoa thamani kwa wengi na hilo litakupa mafanikio makubwa.

Usiogope kutegemewa na wengi kwenye yale makubwa uliyoonyesha unaweza kufanya.
Hilo linakusukuma wewe kufanya kwa ubora zaidi kwa hao walio wengi.
Na hilo litachangia wewe kuweza kufanya makubwa zaidi na zaidi.

Mafanikio yoyote makubwa yanaanzia kwenye kuwa tayari kuwajibika kwa ukubwa na kwa wengi.
Fursa za kuwajibika huko zinapojitokeza, zitumie vizuri ili ziache manufaa makubwa kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe