💯KCM2324081; Yasiyotarajiwa.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#AlhamisiYaUbunifu

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Yasiyotarajiwa.

Leo ikiwa ni #AlhamisiYaUbunifu tunaona jinsi ambavyo ubunifu ni kufanya yale yasiyotarajiwa.

Unapoona watu wanafanya kitu, hata kama ni cha kijinga kiasi gani, kuna namna wananufaika na hicho wanachofanya.

Huwa tunaona watu wengi wakifanya mambo kwa mazoea bila ya kubadilika.
Japo kwenye mazoea hayo wanajizuia kukua na kufanya zaidi, kuna uhakika wanakuwa wanajipa.
Kwenye mazoea ni kwenye ukanda wa ufahari.
Kwenye ukanda huo mtu anakuwa hana wasiwasi mkubwa, kwa sababu anafanya alichozoea kufanya mara zote.
Lakini kwa kuwa anafanya kilichozoeleka, anapata matokeo ambayo ni ya kawaida.

Njia pekee ya kuondoka kwenye mkwamo kama huo ni kubadilika kwenye ufanyaji wako.
Badala ya kufanya yale ambayo umeshazoea kufanya, unatoka nje ya hayo mazoea na kufanya yasiyotarajiwa.

Ubunifu ni matokeo ya kufanya yale yasiyotarajiwa kufanywa.
Na mara nyingi siyo mambo magumu sana kufanyika, ni vile tu watu wameshalewa mazoea na hawaoni kingine nje ya mazoea hayo.

Ili uwe mbunifu na kufanya mambo ya tofauti, lazima kwenye kila unachofanya ujiulize ni yapi ambayo hayatarajiwi kabisa kufanywa, kisha yafanye hayo.
Mwanzo hutapata matokeo kama unayopata kwenya mazoea, lakini kadiri unavyoendelea kufanya, ndivyo matokeo yanavyozidi kuwa ya tofauti na mazuri.

Kwa kila unachofanya, mara zote jiulize ni mambo gani ambayo hayatarajiwi kabisa kufanywa, kisha yafanye hayo kwa uhakika.
Haitakuchukua muda mrefu kabla hujaanza kuzalisha matokeo ya tofauti kabisa na kuwa mbunifu wa kipekee.

Kila mtu ni mbunifu kwa sababu anaweza kufanya yasiyotarajiwa.
Tumia ubunifu wako kuweza kuzalisha matokeo makubwa na ya tofauti.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujiamini na kuamua. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/18/3305

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kufanya yasiyotarajiwa ili kuzalisha matokeo ya tofauti na kuwa wabunifu.

Kocha.
💯