💯KCM2324083; Nafsi.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Nafsi.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo utulivu na upweke vinavyotofautiana kwenye nafsi.
Watu wengi wamekuwa wanachanganya utulivu na upweke.
Kwenye maisha, ili kupata utulivu wa kukuwezesha kutafakari mambo yako, lazima upate muda wa kuwa peke yako.
Pale watu wanapokuwa peke yao, huwa wanachukulia hiyo ni hali ya upweke. Wanaona wamekosa watu wa kuwa nao na hivyo kuona maisha yao hayajakamilika.
Utulivu na upweke zote ni hali za kuwa peke yako bila ya watu wengine.
Lakini hali hizo hazifanani, bali zina tofauti kubwa.
Upweke ni umasikini wa nafsi, unakuwa unataka sana kuwa na watu, lakini huwapati. Hivyo unakuwa peke yako kwa sababu umekosa watu wa kuwa nao. Hilo linakuumiza na kujiona kuna vitu umekosa.
Utulivu ni utajiri wa nafsi, unakuwa umechagua kuwa peke yako kwa kipindi fulani, licha ya kuwa tayari unao watu. Unakuwa peke yako siyo kwa sababu umekosa watu, tayari unakuwa nao wengi, ila unakuwa umejitenga nao kwa muda ili kukamilisha kitu muhimu.
Kuchagua kujitenga na watu kwa muda fulani inakupa utulivu wa kukamilisha yale muhimu.
Mambo yote yanaanza na nafsi yako, jinsi inavyoyachukulia.
Ndiyo maana kwa nje ni vigumu sana kuhukumu kitu kwa usahihi.
Kwa sababu kitu kinavyoonekana kwa nje ni tofauti kabisa na kilivyo ndani.
Nafsi ndiyo inaweza kuelezea kile ambacho inapitia.
Hivyo ni muhimu tusikilize nafsi zetu kwenye kila tunachopitia.
Tujue kama tumechagua hivyo, ambapo inakuwa ni utajiri wa nafsi, au tumelazimika kufanya kwa sababu hakuna namna nyingine, ambapo inakuwa umasikini wa nafsi.
Ukianza na nafsi kwa usahihi, mengine yote yanakwenda vizuri kabisa.
Ielewe nafsi yako na ipe utajiri kupitia utulivu na siyo kuipa umasikini kupitia upweke.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuchagua kwa usahihi. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/20/3307
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuwa na utajiri wa nafsi kwa kuchagua utulivu na siyo kuwa na umasikini wa nafsi unaotokana na upweke.
Kocha.
💯