3308; Usiende kinyume.

Rafiki yangu mpendwa,

Kinachofanya watu wengi kushindwa kupata mafanikio makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wao ni kwenda kinyume na vile wanavyopaswa kwenda.

Yaani unakuta mtu tayari yupo kwenye njia sahihi ya kufanikiwa, lakini anachagua kwenda kinyume na vile anavyopaswa kwenda ili kufanikiwa au kudumu kwenye mafanikio.

Wengi wanapoanza huwa wanakaa kwenye njia sahihi, ambayo inawafikisha kwenye hatua fulani ya mafanikio.
Wakishafika hatua hiyo, wanaanza kwenda kinyume na kujizuia kufanikiwa zaidi na hata kupoteza mafanikio ambayo tayari walishayajenga.

Eneo la kwanza ambalo wengi huenda kinyume ni kwenye kuweka kazi.
Wakiwa wanaanza wanaweka kazi kubwa. Wakipiga hatua wanapunguza kuweka kazi. Matokeo yake ni kushindwa kupiga hatua kubwa na hata kurudi nyuma.
Kazi yoyote unayokuwa umeweka na ukapiga hatua, unatakiwa kuweka kiwango hicho hicho cha kazi kubaki kwenye hatua hiyo. Na kama unataka kupiga hatua zaidi ya hiyo, kazi unatakiwa kuweka mara mbili zaidi.
Usiende kinyume na hilo kwenye kazi, utajipoteza mwenyewe.

Eneo jingine la kuepuka kwenda kinyume ni watu. Mafanikio yoyote unayoyataka yanahitaji sana watu. Kadiri unavyopiga hatua kubwa zaidi, ndivyo unavyohitaji watu wengi zaidi. Hivyo zoezi la kutengeneza watu wengi zaidi kwenye safari yako linapaswa kuwa endelevu.

Ujuaji ni mahali pengine panapowaangusha wengi.
Wanapoanza wanakuwa tayari kujifunza kila kitu. Hilo linawasukuma kuwa na ukuaji mkubwa. Wakishapiga hatua fulani wanajiona wameshajua kila kitu na hawana tena cha kujifunza. Na hapo ndipo ukuaji unapokwama na hata anguko kuanza.

Kwa kifupi ni chochote kinachokupa mafanikio, unapaswa kuendelea kukifanya kwa ukubwa zaidi hata baada ya kufanikiwa.
Kamwe usiache kile kilichokuinua, maana kufanya hivyo ni kukaribisha anguko kubwa kwako.

Huwa kuna kauli inayosema kile kinachokupandisha ndicho pia kinachokushusha. Kitu kinakupandisha pale unapokifanya kwa usahihi. Na kinakushusha pale unapokifanya kwa makosa au kutokukifanya kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe