💯KCM2324084; Marekebisho.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Marekebisho.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii ni ya kufanya marekebisho kwenye makosa mbalimbali unayokuwa umefanya kwenye siku nyingine za wiki.
Kwenye maisha, unapokuwa kwenye kasi, unachoangalia ni kule unakokwenda tu.
Ni vigumu sana kuangalia nyuma na kuona makosa uliyofanya ili kuyarekebisha.
Unaweza kuangalia nyuma pale unapopunguza kasi unayokuwa nayo.
Na hilo ndiyo linafanya mapumziko kuwa muhimu kwenye safari zetu za maisha.
Mtu unaweza kuona kupumzika ni kupoteza muda, lakini hilo siyo sahihi.
Kupumzika ni kujiandaa kuutumia vizuri muda ujao, kwa kurekebisha yale ya nyuma ambayo yalivuruga matumizi ya muda.
Kama ambavyo wafanya mazoezi makali ni lazima wawe na mapumziko, kwa sababu ni wakati wa mapumziko ndiyo misuli hujengeka.
Kadhalika ili tuweze kutumia siku zetu za wiki, tunapaswa kuifanya siku moja kuwa ya mapumziko.
Kadhalika, tunapolala ndiyo mwili unatumia hiyo nafasi kufanya marekebisho mbalimbali.
Ndivyo pia siku ya mapumziko inavyokuwa ya kufanya maboresho ya siku nyingine za mchaka mchaka.
Kinachoonekana kuwa upotevu wa muda ndiyo kinachochangia matumizi bora zaidi ya muda.
Kwenye maisha, kila mtu anakosea.
Tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni uharaka wa kufanya marekebisho kwenye makosa.
Wakati wanaofanikiwa wakirekebisha makosa yao haraka, wanaoshindwa wanakuwa wanayarudia kwa muda mrefu.
Ili uweze kurekebisha makosa kwa haraka, lazima uweze kuyaona kwa haraka pia. Na njia pekee ya kuyaona makosa kwa haraka ni kuwa na mapumziko ambayo unayatumia kutafakari hatua zote ambazo umepiga.
Hapo tunaona jinsi ya kuhakikisha mapumziko hayawi upotevu wa muda.
Kwa kuhakikisha unayatumia mapumziko kutathmini mwenendo wako mzima na kuona ni maeneo yapi ambayo unahitaji kufanya maboresho ili safari yako iwe kama unavyotaka.
Kukimbia kwa kasi wakati umeshapoteza mwelekeo haikufanyi kuwahi popote, bali inakupoteza kabisa.
Kuwa na mapumziko ya kujifanyia tathmini na kuona marekebisho ya kufanya ili uweze kupata kile hasa unachotaka.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu usiende kinyume. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/21/3308
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kutafakari na kutathmini mwenendo wako mzima na kuona maeneo ya kurekebisha ili upate kile unachotaka kwa uhakika.
Kocha.
💯