3309; Okoa hizo nguvu.

Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya kanuni za fizikia ni uhifadhi wa nguvu.
Kanuni hiyo inasema nguvu haiwezi kutengenezwa wala kuharibiwa, bali inaweza kubadilishwa kutoka hali moja kwenda nyingine.

Kanuni hii inagusa kila eneo la maisha yetu, hasa kwenye miili yetu.
Kama unakosa nguvu za kuyapambania mafanikio yako, siyo kwa sababu huna, bali ni kwa sababu unazitumia kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

Unachopaswa kufanya ni kuhamishia nguvu hizo kwenye mambo yenye tija kwako.

Kwa mfano eneo ambalo huwa linachukua nguvu za watu wengi ni la kuongea.
Watu wamekuwa wanaongea sana, kiasi kwamba ukifika wakati wa kuchukua hatua, wanakuwa wameshachoka.
Wewe kuwa tofauti, okoa hizo nguvu kwa kuacha kuongea na kwenda moja kwa moja kwenye hatua.
Matokeo utakayozalisha yataongea kwa sauti kuliko unavyoweza kuongea wewe.
Hapo utakuwa umepata unachotaka na imesikika.
Lakini ukikazana kusema wewe, na hata kubishana, utachoka sana, utakosa nguvu za kufanya na wale waliokuwa wanakubishia watakuwa sahihi.

Kuhangaika na mambo ya wengine nako ni matumizi mabaya ya nguvu zako.
Unaweza kuona unapaswa kuwasaidia wengine kwenye mambo mbalimbali wanayopitia.
Lakini usichojua ni wengi hawahitaji kabisa msaada wako.
Kwa sababu hayo unayoona wanayapitia, wameyatengeneza wao wenyewe kama sehemu ya kutoroka ili wasiwajibike kwenye maeneo mbalimbali ambayo wamepwaya.
Hivyo wakati wewe unakazana kuwasaidia, na wao ndiyo wanazidi kuharibu.
Hivyo unaishia kuhamisha nguvu ambazo ungezitumia vizuri ungefanya makubwa.

Peleka nguvu zako zote kwenye mambo yenye tija kwako.
Na namba moja ikiwa ni lengo lako kuu unalopambania.
Mengine yote yanapaswa kusubiri.
Kwa njia hiyo utaweza kufanya makubwa na kupata unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe