3310; Msukumo wa kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli inayosema hatima ya yai ni kuvunjika.
Na matokeo ya kuvunjika kwa yai huwa yanategemea chanzo cha nguvu ya kuvunja yai hilo.
Kama yai litavunjwa kwa nguvu inayotoka nje, huwa ni mwisho wa uhai wake.
Lakini kama yai litavunjwa kwa nguvu inayoanzia ndani, huwa mwisho wake ni maisha mapya, yaani kupatikana kwa kifaranga.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye msukumo wa watu kuchukua hatua kwenye maisha.
Hatima ya msukumo wa watu kuchukua hatua huwa inategemea na chanzo cha msukumo huo.
Pale msukumo wa mtu kuchukua hatua unapoanzia ndani yake, hatima yake huwa ni mafanikio makubwa.
Lakini pale msukumo wa mtu kuchukua hatua unapotoka nje yake, hatima yake huwa ni matokeo ya kawaida.

Kutegemea msukumo wa nje ndiyo mtu uchukue hatua ni kujikwamisha kupata mafanikio makubwa.
Hiyo ni kwa sababu safari ya mafanikio ni ngumu na yenye vikwazo mbalimbali, kama mtu hajajitoa kweli kweli, hawezi kuvivuka hivyo na kufanikiwa.

Msukumo wa ndani huwa una nguvu kubwa zaidi na hauchoki haraka.
Ni msukumo unaowafanya watu kuweka juhudi kubwa zaidi na kwa muda mrefu bila ya kukata tamaa.

Msukumo wa ndani ndiyo unamfanya mtu kuchukua hatua mara moja kwenye kila linalotokea, bila ya kusubiri kwa muda mrefu.
Wenye msukumo wa ndani hawasubiri mpaka wapate taarifa zaidi na kujadiliana na wengine ndiyo wachukue hatua.
Wao huchukua hatua mara moja pale inapohitajika kufanya hivyo, bila ya kusita sita.

Ni msukumo huo wa kuchukua hatua na kufanya ndiyo unawatofautisha wanaopata mafanikio makubwa na wanaoishia kuwa kawaida.

Jitafakari wewe mwenyewe huwa msukumo wako wa kufanya vitu unaanzia wapi?
Kama ni ndani yako, basi endelea kuutumia kwa sababu utapata matokeo makubwa.
Na kama msukumo ni wa nje, tafuta kile kitakachoamsha msukumo wa ndani yako, kwa sababu kwa msukumo wa nje huwezi kufanya makubwa.

Kadhalika kwa watu unaoshirikiana nao kwa namna mbalimbali. Angalia wale ambao tayari wana msukumo wa kufanya ndani yao. Hawa hawahitaji uangalizi wa karibu sana.
Lakini ukishirikiana na ambao wanahitaji msukumo wa nje ndiyo wafanye, utahitajika kuwasimamia kwa karibu sana. Na bado matokeo yao yatakuwa ya kawaida sana.

Kama msukumo wa ndani haupo kwa mtu, mbegu ya kujenga mafanikio makubwa pia inakuwa haipo.
Hili ni eneo ambalo kil mtu anapaswa kulifanyia kazi kwa uhakika ili lisiwe kikwazo kwa mafanikio yao makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe