Huwa kuna utani kwamba kitu pekee ambacho watu wanajua kwa uhakika kuhusu fedha ni jinsi ya kuzitumia. Ukimpa tu mtu fedha, huhitaji hata kumpa darasa lolote, ataweza kuzitumia kwa haraka sana na kuzimaliza zote.
Lakini inapokuja kwenye kutengeneza fedha, hasa kwa utajiri mkubwa, watu wengi hawana uelewa wowote. Na hata kwa wale ambao wanasukumwa na mahitaji yao ya kuwa na fedha zaidi, huwa wanakazana kuongeza kipato.
Wengi wanapokazana kuongeza kipato wanakuwa wanadhani kwamba wakishakuwa na fedha nyingi, matatizo yao yote yataisha. Kinachokuja kuwashangaza ni pale wanapokuwa wamepata fedha nyingi na matatizo yao kuwa yameongezeka zaidi kuliko kupungua.

Ongezeko la fedha huwa linakuja na ongezeko la matatizo pale watu wanapokuwa wamekosa elimu sahihi ya jinsi ya kutunza na kukuza utajiri. Matokeo yake ni wale wanaojenga utajiri huwa wanaishia kuupoteza, kama siyo wakiwa hai, basi baada ya kifo chao utajiri wote unapotea.
Siri moja muhimu sana kuhusu utajiri ambayo imekuwa haifundishwi kwa wengi ni kwamba utajiri ni kile kisichoonekana. Watu wasio na mafunzo sahihi ya utajiri huwa wanakimbilia kuwa na matumizi makubwa pale kipato chao kinapoongezeka. Matokeo yake ni kujikuta wanakaribisha matatizo na changamoto nyingi.
Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanapenda fedha kwa urahisi. Hivyo kwa yeyote ambaye kwa nje anaonekana kuwa na fedha, huwa anawindwa na hao wengi wanaotaka kujipatia fedha hizo. Ndiyo maana ni siri muhimu sana kwamba utajiri wako mkubwa unapaswa kuwa usioonekana au kushikika.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha kwa kina kuhusu dhana hii ya utajiri ni kile kisichoonekana na kwa nini ni muhimu sana ufanye hivyo. Pia nimekushirikisha jinsi ya kutekeleza hili ili unapojenga utajiri uwe na utulivu mkubwa wa maisha yako. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.