Fursa za biashara ni nyingi, kwenye kila sekta huwa kuna biashara kubwa ambazo zimetawala sehemu kubwa ya soko na kuaminiwa na wateja. Kutokana na biashara hizo kuwa na wateja wengi, huwa zinashindwa kuwahudumia vizuri. Matokeo yake ni wateja kuwa na malalamiko mbalimbali.
Hapo watu huona fursa na kuanzisha biashara ambazo zinatatua malalamiko yaliyopo kwenye hizo biashara kubwa. Biashara hizo zinakuwa na msukumo mkubwa mwanzoni wa kuwapa wateja huduma nzuri ambazo hawapati kwenye biashara kubwa. Wateja wanaipenda biashara mpya na kuambiana na hilo linapelekea biashara hiyo kupata wateja wengi zaidi.

Ni pale biashara inapopata wateja wengi ndiyo mambo huwa yanaanza kulalamika. Kwanza inashindwa kuwahudumia vizuri, kitu ambacho kinaleta yale malalamiko yaliyokuwepo kwenye biashara kubwa. Na pili, wamiliki wanakuwa wameanza kupata fedha nyingi na hivyo hawana tena ule msukumo waliokuwa na awali.
Matokeo ya hilo ni biashara kuwa kama zile kongwe ambazo zina malalamiko na hazina ukuaji. Mafanikio ya kasi yaliyopatikana yanafifia na anguko linafuata. Hivyo ndivyo biashara nyingi zinavyoanza, kufanikiwa na kuanguka.
Kama unaanza au tayari upo kwenye biashara, kuna namna ya kuzuia biashara yako isiende kwenye hiyo njia ambayo inaishia kwenye anguko. Njia hiyo ni kuifanya kila siku ya biashara yako kuwa kama siku ya kwanza. Hapo unaiendesha biashara yako kwa ile kasi ya mwanzo bila ya kuridhika.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kuifanya biashara kila siku kama siku ya kwanza. Karibu usikilize kipindi na uondoke na hatua za kwenda kuchukua ili ujenge biashara itakayokuwa na mafanikio yanayodumu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.