3312; Hatua na matokeo.

Rafiki yangu mpendwa,

Matokeo tunayoyapata mwenye maisha yanatokana na hatua tunazochukua.
Lakini watu wengi huwa wanasahau hilo na kuyaangalia matokeo yenyewe.
Na kama matokeo hayawafurahishi, hawajitathmini kwenye hatua walizochukua, bado wanaangalia nini kingine wafanye ili kupata matokeo wanayotaka.

Mara nyingi sana, pale mtu anapokosa matokeo aliyokuwa anayataka, mahali pa kuanzia siyo hatua gani nyingine za kuchukua, bali ni usahihi wa hatua zilizochukuliwa.
Kwa uvivu wetu binadamu huwa hatuchukui hatua kwa usahihi wake.
Badala yake tunachagua nini cha kufanya, ambacho hakituumizi sana.
Na hapo tunajua, kufanya ambacho hakikuumizi ni kupata matokeo ya kawaida.

Kwenye ushauri ambao watu wanaomba nako kuna vitu vya kushangaza.
Watu wanachukua nusu ya ushauri waliopewa…
Wanaenda kufanyia kazi nusu ya ushauri huo…
Halafu wanashangaa pale matokeo wanayopata ni tofauti na yaliyoelezwa kwenye ushauri.

Kama hujafanyia kazi ushauri uliopewa, kwa hatua zote ulizoshauriwa, hupaswi kushangaa pale matokeo yanapokuja tofauti.
Kama umeamua kuchagua machache unayofanya kwenye ushauri ukiopewa, basi pia pokea matokeo yoyote yatakayokuja.

Kilicho sahihi kwenye ushauri unaopewa ni kuufanyia kazi kwa usahihi kwanza kabla ya kusema ushauri huo haufanyi kazi.
Na kwa matokeo yoyote unayoyapata, kama hayakuridhishi, anza kwa kuangalia hatua ulizochukua.
Mara nyingi utakuta kuna namna uchukuaji wako wa hatua unaathiri matokeo unayoyapata.

Hakikisha kwanza umechukua hatua kwa usahihi kabla hujahangaika na kuzibadili hatua hizo.
Ukianzia kwenye huo msingi, kuna mengi ambayo utaona ya kurekebisha kabla ya kwenda kwenye vitu vipya kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe