3314; Muda na usumbufu.
Rafiki yangu mpendwa,
Imekuwa ni kawaida kwa watu kusema kama wangepata muda zaidi basi wangeweza kufanya makubwa.
Hiyo imekuwa ni njia nyingine ya watu kuonyesha kwamba kinachowakwamisha ni ufinyu wa muda.
Lakini tunajua ukweli kwamba muda uliopo ni sawa kwa kila mtu.
Kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kupata muda wa ziada.
Sasa kama kila mtu ana muda sawa na kuna ambao wanaweza kutumia muda huo kufanya makubwa, wanaokwama sababu haiwezi kuwa ufinyu wa muda.
Sababu kuu ya wale wanaoshindwa kufanya makubwa kwenye muda walio nao ni yale wanayochagua kufanya kwenye huo muda.
Wanaoshindwa kufanya makubwa wanatumia muda wao kufanya mambo yasiyokuwa na tija.
Kwa maneno mengine wanatumia muda huo kuhangaika na usumbufu badala ya kuhangaika na yale yenye tija.
Wale wanaofanya makubwa wanalinda sana muda wao kwa kufanya yale tu yenye tija.
Kwa njia hiyo wanajikuta wakikamilisha makubwa na kupiga hatua zaidi.
Kwa maana hiyo basi, unachohitaji siyo kupata muda zaidi, bali kupunguza usumbufu.
Huwezi kupata muda wa ziada, kwa sababu wote tumepewa muda sawa.
Lakini unaweza kuzuia kupoteza muda wako kwenye mambo yasiyokuwa na tija.
Acha kufanya jambo lolote ambalo halina mchango kwako kufika kule unakotaka kufika.
Kuwa bahili sana wa muda wako, usikubali kuupoteza wala kuruhusu wengine wauchezee.
Pangilia muda wako vizuri kwa yale yenye tija tu.
Na fuata muda wako kama ulivyoupangilia ili kufanya yale yenye tija.
Kwenye muda, usijidanganye kwamba utapata muda zaidi, bali kuwa mkweli kwako mwenyewe kwenye matumizi ya muda wako. Ukiuelekeza muda kwenye yale yaliyo sahihi tu, utaweza kufanya makubwa sana.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Asante sana kocha nitafanya yale yenye tija tu ili niwe na muda wa ziada
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike