💯KCM2324090; Kuchagua.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Kuchagua.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo kuweza kuchagua kile unachofanya ni uhuru unaotokana na mtu kuweza kujitegemea.
Kwenye maisha, huwa tuna namna mbili za kufanya kitu chochote kile.
Inaweza kuwa tunalazimika kufanya, hapa tunafanya kwa sababu hatuna namna nyingine.
Mambo ambayo unalazimika kufanya iwe unapenda au hupendi yanatokana na vitu tunavyokuwa tunawategemea watu wengine.
Kwa kuwa unawategemea wengine, inakubidi ufanye kile wanachotaka ufanye, ndiyo uweze kupata kile unachotaka.
Kwa upande wa pili kuna mambo ambayo unajitegemea wewe mwenyewe.
Kwa haya unayafanya kwa sababu umechagua wewe mwenyewe kuyafanya.
Kwa kuwa hakuna anayekulazimisha kufanya, unafanya kwa sababu ni muhimu kwako na ndiyo yenye tija.
Kwa bahati mbaya sana, tulitegemea kwa yale mambo ambayo mtu yupo huru kufanya ndiyo ayafanye vizuri na yampe manufaa.
Lakini kwa kukosa utulivu, wengi hushindwa kutumia nafasi hiyo vizuri na kuishia kutumia uhuru wanaokuwa wameupata vibaya.
Kwa yale ambayo watu wanalazimika kufanya, huwa wanayafanya hata kama hawataki. Na hayo ndiyo yamekuwa yanawapa matokeo ambayo ni makubwa.
Chagua kuwa na utulivu mkubwa sana ndani yako ili uweze kutumia uhuru unaokuwa nao kuchagua kufanya yale yenye tija, kitu ambacho kitakupa uhuru zaidi na zaidi.
Kama utashindwa kutumia vizuri hata uhuru mdogo ulionao, utazidi kuupoteza uhuru huo na kujikuta ukizidi kuwa tegemezi na kulazimika kufanya mengi ambayo hutaki kuyafanya.
Wengi tunaanza tukiwa na mengi ambayo tunalazimika kufanya, kwa sababu hatuna namna nyingine.
Wanaofanikiwa sana ni wale wanaoenda wakipunguza wanayolazimika kufanya na kuongeza wanayochagua kufanya. Wanakuwa wanakuza uhuru wao zaidi na zaidi.
Wanaoshindwa wanakuwa wanazidi kupoteza uhuru wao kwa kuzidi kulazimika wasiyotaka kufanya.
Jua unapoanzia na elekea upande wa kuchagua zaidi kuliko kulazimika.
Na hilo linataka uwe na utulivu mkubwa sana na kufanya yale tu yenye tija kwako na kukutoa kwenye utegemezi wa wengine.
Kwa kila unachofanya, hakikisha unajenga uhuru zaidi ili kuchagua kufanya na siyo kulazimika kufanya.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu muda na usumbufu. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/27/3314
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujijengea utulivu mkubwa na kufanya yale unayochagua na siyo unayolazimika kufanya.
Kocha.
💯