💯KCM2324091; Upya.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumapiliYaMapumziko

Mwanamafanikio,

Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.

Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.



💯 Neno la leo; Upya.

Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii ni ya kuwa na mtazamo wa kuanza upya bila kujali nini umepitia kwa wiki nzima.

Kwenye maisha, hakuna kitu kinachotokea kwa mara moja.
Kila kitu huwa kinaanza kidogo kidogo na kwa muda mrefu, kisha baadaye kinatokwa kwa ukubwa na haraka.

Hakuna anayepotea mara moja, bali mtu anakuwa anapotea kidogo kidogo kwa muda mrefu. Anakuja kushtuka ameshapotea mbali sana na hapo kukata tamaa kwamba hawezi tena kurudi kwenye njia sahihi.

Ndiyo maana ni muhimu sana kwenye kila safari, kila mara kujiangalia kama bado upo kwenye njia sahihi au umeanza kupotea.
Unapojikagua mara kwa mara, unapata nafasi ya kujua ni wapi upo na hatua zipi za kuchukua ili kurudi kwenye njia sahihi.

Kwenye safari yetu ya maisha, tuna siku saba za wiki, ambapo siku sita ni za kufanya kazi na siku ya saba ikiwa ya mapumziko.
Siku hiyo ya mapumziko ni muhimu sana kwa sababu ndiyo maalumu kwa ajili ya kujikagua kama bado upo kwenye njia sahihi.

Pale unapojikagua na kugundua haupo kwenye njia sahihi, anza upya kwa kurudi kwenye mpango mkuu na kuchukua hatua zilozo sahihi.
Unapokuwa hujapotea sana, kubadilika inakuwa rahisi.
Hivyo kujikagua kila mara ni muhimu.

Unapaswa kuitumia kila siku ya jumapili kama siku ya kuanza upya.
Siku ya kuondoa wasiwasi na hofu zinazokukwamisha kufanya makubwa.
Ifanye kuwa siku ya kukagua vikwazo vinavyokuzuia na kuweza kuvivuka kwa uhakika.

Unapokuwa kwenye kasi, ni vigumu kuangalia nyuma na kujua kama bado upo kwenye njia sahihi.
Ni pale unapopunguza mwendo ndiyo unaweza kujitathmini mwenendo wako na hatua sahihi za kuchukua ili kurudi na kubaki kwenye njia kuu.

Wakati mwingine unakuwa umekusanya vikwazo vingi sana kiasi cha kuona huwezi tena kuendelea.
Lakini unapojipa nafasi ya kuanza upya, unaachana na hayo yote na kuchukua hatua sahihi na zinazokupa kile unachotaka.

Itumie kila jumapili yako kwa usahihi, ili uweze kuanza upya kwenye yale yote unayokuwa umekwama.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ugumu wa kuanza. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/28/3315

Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kuanza upya kwenye maeneo yote unayokuwa umekwama au kupotea kwenye kuendea kile unachotaka.

Kocha.
💯